NA MWANDISHI MAALUM, WyEST
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii imeutaka uongozi wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST) kuendeleza bunifu za wanafunzi wa chuo hicho pamoja na kulinda maslahi ya wabunifu hao ili ubunifu wao uweze kutambulika na kumnufaisha mbunifu na Taifa.
Hayo yamesemwa mkoani Mbeya na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Stanslaus Nyongo (Mb) mara baada ya kamati hiyo kukagua miradi ya ujenzi na kuoneshwa ubunifu mbalimbali wa wanafunzi wa chuo hicho.
"Mbali ya miradi ya ujenzi tuliyokagua, tumevutiwa sana na baadhi ya bunifu za wanafunzi wa chuo hiki. Uongozi wa chuo hakikisheni mnalinda maslahi yao ili kuwe na utambulisho rasmi kuwa teknolojia au bidhaa hii imebuniwa na mwanafunzi fulani hatimae imnufaishe yeye na Taifa," amesema Mhe. Nyongo.
Katika hatua nyingine Kamati hiyo imekitaka chuo hicho kuongeza idadi ya udahili wa wanafunzi wa kike na kukishauri kutumia kitengo chake cha masoko kuhamasisha kuhusu suala hilo.
"Tumeona katika taarifa yenu idadi ya wanafunzi wa kike ni ndogo, tunasisitiza watoto wa kike wahamasishwe kujiunga na chuo hiki kwa kutumia kitengo cha masoko," amesisitiza Mhe. Nyongo.
Naye Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Omari Kipanga (Mb) akiongea kwa niaba ya Waziri Mhe. Adolf Mkenda amesema kupitia fedha za mradi wa HEET chuo cha MUST kimetengewa jumla ya Shilingi bilioni 41.2 ambazo zitatumika kuboresha miundombinu ya chuo hicho.
"Ni kweli tuna changamoto ya upungufu wa watoto wa kike katika kozi za sayansi chuoni hapa, lakini kupitia shule za sekondari zaidi ya 25 za wanafunzi wa kike za mchepuo wa sayansi zinazojengwa na Serikali, tunaamini tutapata watoto wengi watakaojiunga na vyuo vya sayansi kikiwemo hiki cha MUST," amefafanua Mhe. Kipanga.
Ameongeza kuwa wamepokea maelekezo na ushauri wote uliotolewa na Kamati hiyo na kuahidi kwenda kuyafanyia kazi kwa kushirikiana na Wizara.