>Waomba katazo hilo lipitiwe upya ili kufungua fursa za ajira
NA HADIJA BAGASHA
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma (PIC) imejia juu katazo la kusafirisha viumbe hai nje ya nchi jambo ambalo limewaathiri wafugaji wa vipepeo katika milima ya Amani wilayani Muheza mkoani Tanga.
Kamati hiyo pia ilijionea miradi mbalimbali ndani ya hifadhi hiyo inayotekelezwa na TFS katika msitu huo jambo ambalo ilionyesha kuridhishwa.
Kauli hiyo imetolewa na mwenyekiti wa kamati hiyo, Jerry Silaa wakati wa ziara ya kamati hiyo ilipotembelea Hifadhi ya Msitu wa Asili wa Amani uliopo wilayani Muheza mkoani Tanga ambapo amesema ipo haja ya serikali ipitie sheria hiyo na kuangalia namna ambavyo wananchi waliokuwa wanafuga vipepeo na kuwauza nje nchi kwa ajili ya kujipatia kipato wameathirika.
Wakiwa kwenye hifadhi hiyo wabunge pamoja na mambo mengine wamezungumzia zuio hilo la usafirishaji wa vipepeo nje ya nchi kitendo ambacho kimewaathiri wazalishaji ambapo wameitaka wizara husika kulifanyia marekebisho jambo hilo.
"Niseme tu kwamba serikali ilitoa katazo baada kuingia dosari ya kusafirisha viumbe wengine zaidi ya vipepeo, hivyo tunapendekeza ipitie sheria hiyo ili kuendeleza ufugaji wa vipepeo kwa wananchi na kujiongezea vipato vyao,"amesema Silaa.
"Tumejionea mambo mengi tukiwa katika hifadhi hii, aina mbalimbali za miti ambayo inapatikana hapa, ujenzi wa miundombinu ya barabara pamoja na njia za watembea kwa miguu na majengo na tumefurahishwa,"amesema Silaa.
Sambamba na hayo wajumbe wa kamati hiyo wameridhishwa na matumizi ya fedha za Serikali zilizotolewa kwa ajili ya maboresho ya miundombinu ya barabara na majengo.
Kwa upande wake Kamishna wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TSF),Prof. Dosantos Silayo amesema suala la ufugaji wa vipepeo kwa wakazi wa eneo la amani wamepokea maelekezo ya Kamati hiyo na kwamba watalifikisha wizarani.
Prof.Silayo amezitaja fursa zinazopatikana katika misitu hiyo kuwa ni utalii wa misitu kilimo cha viungo pamoja na ufugaji wa vipepeo.
Aidha, amesema kuwa pia tasisi hiyo imejikita katika kutoa elimu ya uhifadhi wa mazingira kwa wananchi wanaoishi pembezoni wa misitu hiyo.