NA MWANDISHI DIRAMAKINI
ZIARA ya kutembelea wananchi wa kata na vijiji mbalimbali ya Mbunge wa Chalinze na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Ridhiwani Kikwete imefika Kata ya Kibindu huku wananchi wakiishukuru Serikali pamoja na mbunge huyo kwa namna ambavyo amekuwa mstari wa mbele kuwatetea ili kupata maendeleo.
Hussein Shafii wakati akizungumza mbele wa Mhe.Ridhiwani kwenye mkutano huo amesema,wanamshukuru Mhe. Mbunge wa Naibu Waziri kwa kutatua mgogoro wa kwenye Hifadhi ya Uzigua kwenye Kijiji cha Kwa-Mduma.
Naye Selemani akapongeza jitihada za Mhe.Ridhiwani kusukuma ukarabati wa barabara kila mara ikiharibika huku sasa hivi ikijengwa barabara kubwa kutoka kwa Luhombe mpaka Gole ambayo Mkandarasi yuko kazini anajenga barabara hiyo kwa kasi.
Wakatati huo huo, wananchi wa kata hiyo wamemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan na Mhe.Ridhiwani kwa kufanikisha kujenga Kituo cha Afya Kibindu ambapo Rais Samia alileta fedha pamoja na ununuzi wa gari ya kubebea wagonjwa.
Wamesema,usimamizi wa Mhe.Ridhiwani ulipelekea serikali kutoa kiasi cha shilingi Bilioni 1.8 kwa ajili ya ujenzi wa mabwawa mawili makubwa ya maji katika Kitongoji cha Mjema na lingine kijiji cha Kwa-Msanja ambayo yatasaidia kupeleka maji na kumaliza changamoto ya maji kwenye vijiji vya Kata ya Kibindu na hususan vijiji vya Kwa- Mduma, Kibindu, na hasa kitongoji cha Kwa-Vuli na kadhalika.
Kwenye mikutano hiyo, wananchi pia walipata nafasi ya kueleza changamoto na kero zao ambazo papo kwa papo zilipatiwa ufumbuzi na Mhe.Ridhiwani Kikwete na wataalamu mbalimbali wa Halmashauri ya Chalinze wakiongozwa na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo.