KUELEKEA MWAKA MMOJA WA UONGOZI WA RAIS SAMIA:Bilioni 662.32/- zaleta mageuzi chanya Sekta ya Elimu nchini

NA GODFREY NNKO

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mheshimiwa Innocent Bashungwa amesema,Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan imevunja rekodi ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya elimu kwa kipindi kifupi cha uongozi wake.
Mheshimiwa Bashungwa ameyasema hayo leo Machi 1, 2022 wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma kuelezea mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita kwa kipindi cha kuanzia mwezi Machi 2021 hadi Januari 2022 kuelekea mwaka mmoja wa uongozi wa Rais Samia madarakani.

"Katika Serikali ya Awamu ya Sita kwa kipindi cha kuanzia mwezi Machi 2021 hadi Januari 2022, yaani miezi 11 kabla ya hata kukamilisha mwaka mmoja tangu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan aingie madarakani, Ofisi ya Rais- TAMISEMI imepokea jumla ya shilingi trilioni 1.49 kwa ajili utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika Sekta ya Elimu, Afya na Barabara,"amefafanua Mheshimiwa Bashungwa.

Amesema, katika Sekta ya Elimu fedha zilizopokelewa kwa kipindi hicho ni shilingi bilioni 662.32 ambazo zimetumika kutekeleza shughuli mbalimbali kwa ufanisi na matokeo makubwa.

"Kupitia fedha hizo, tumeweza kujenga shule mpya 257 za sekondari na shule tisa za msingi vikiwemo vyumba vya madarasa 18,219 kwa shule za msingi, vituo shikizi na shule za sekondari.

"Pia kupitia fedha hizo tumewezesha kukamilisha ujenzi wa vyumba vya madarasa 4,525 kwa shule za msingi na sekondari ikiwemo kukamilisha ujenzi wa vyumba vya maabara 1,399 nchini,"amesema Mheshimiwa Waziri Bashungwa.

Ameendelea kufafanua kuwa, kupitia fedha hgizo wamewezesha kukamilisha matundu ya vyoo 568 kwa shule za msingi na sekondari ikiwemo kukamilisha mabweni 170 kwa shule za msingi na sekondari.

Sambamba na kukamilisha nyumba za walimu 42 kwa shule za msingi na sekondari. "Pia tumewezesha kukamilisha maabara 11 kwa shule za sekondari na mabwalo sita kwa shule za sekondari,"amebainisha Mheshimiwa Waziri Bashungwa.

Mafanikio mengine, Mheshimiwa Waziri amesema,wameweza kukamilisha majengo ya utawala manne kwa shule za sekondari na kukamilisha Shule Kongwe nne zikiwemo za shule msingi na sekondari.

Wakati huo huo amesema kuwa, katika Sekta ya Elimu fedha ambazo zinatarajiwa kupokelewa kwa kipindi cha Machi hadi Juni, 2022 ni shilingi bilioni 72.96 ambazo zitatumika kutekeleza shughuli mbalimbali katika Sekta ya Elimu.

Mheshimiwa Waziri Bashungwa amezitaja shughuli hizo kuwa ni ujenzi wa vyumba vya madarasa 300 elimu ya awali vya mfano kwa shule za msingi ikiwemo ukamilishaji wa ujenzi wa vyumba vya madarasa 3,468 kwa shule za msingi na sekondari.

"Pia fedha hizo zitatumika kukamilisha ujenzi wa vyumba vya maabara 221, mabweni 20 ya wanafunzi wenye mahitaji maalum na ukarabati wa vituo vya walimu 346 vya shule za msingi na kuongeza miundombinu madarasa ya kidato cha tano na sita katika shule 10 za sekondari,"amefafanua Mheshimiwa Waziri Bashungwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news