NA TITO MSELLEM-WM
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameanza uongozi wake kwa kusaidia na kuvutia wawekezaji ambapo Dunia imeshuhudia wawekezaji wakija kwa wingi kuweza nchini.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nauye ambaye alikuwa Mgeni Rasmi katika hafla ya kuchambua Kurasa 365 za Mama iliyofanyika katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.
Nauye amesema, katika kipindi cha mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imeendeleza mazuri yote yaliyoachwa na uongozi wa awamu tano zilizopita na amerekebisha maeneo yenye makosa kwa lengo la kukuza uchumi wa nchi na kuondoa utegemezi.
Akizungumzia Mafanikio ya Wizara ya Madini na Taasisi zake, Kaimu Kamishna Msaidizi wa Uendelezaji Migodi Theresia Ntuke amesema, Serikali ya Awamu Sita imeacha alama kubwa katika kipindi cha mwaka mmoja wa Rais Samia Suluhu Hassan madarakani ambapo Sekta ya Madini imezidi kukua na kuimarika zaidi.
Ntuke amesema, chini ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita, mchango wa Sekta ya Madini katika Pato la Taifa umekuwa ukiongezeka kutoka robo moja ya mwaka hadi nyingine ambapo amesema katika kipindi cha Januari- Septemba, 2021 wastani wa mchango wa sekta hiyo umekuwa hadi kufikia asilimia 7.3 ya Pato la Taifa ikilinganishwa na wastani wa asilimia 6.5 katika kipindi kama hicho mwaka 2020.
Pamoja na mambo mengine Ntuke amesema, katika kipindi cha mwaka mmoja wa uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita, Sekta ya Madini imefanikiwa kupata mauzo ya moja kwa moja yenye thamani ya shilingi trilioni 8.3 kutokana na madini ya aina mbalimbali.
Kwa upande wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Deusdedith Magala kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo Dkt. Vanance Mwasse amesema, katika mwaka mmoja au Siku 365 za Mama, Shirika hilo limefanikiwa kuongeza mapato ya ndani kutoka shilingi bilion 15.58 kwa mwaka uliopita hadi kufikia bilioni 22.34, Machi 2022 sambamba na kutoa gawio la shilingi bilioni 1 serikalini.
Aidha, Magala ameeleza mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha Awamu ya Sita ni pamoja na ujenzi na ufunguzi wa kiwanda kikubwa cha ubia cha kusafisha madini ya dhahabu cha Mwanza Precious Metals Gold Refinery chenye uwezo wa kusafisha kilo 480 za dhahabu kwa siku kwa kiwango cha kimataifa cha asilimia 999.9.
Pia, Magala amesema Shirika limenunua mitambo ya kisasa nane (8) ya uchorongaji na kupata kandarasi za uchorongaji zenye jumla ya shilingi bilioni 24.3 ukilinganisha kandarasi zenye thamani ya Shilingi bilioni 9.34 za mwaka uliopita.
Magala ameainisha mafanikio mengine yakiwemo kuanzisha mradi wa kutengeza mkaa mbadala unaotokana na makaa ya mawe (Coal Briquttes), kuboresha vituo vya mfano vya wachimbaji wadogo na kuwaunganisha na taasisi za kibenki na pia, maboresho makubwa yamefanyika katika Vituo vya Mfano vya Lwamgasa, Katente na Itumbi.