Madaktari bingwa kutoka India kuweka kambi Zanzibar

NA KHADIJA KHAMIS-MAELEZO

WAZIRI wa Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto, Mhe.Nassor Ahmed Mazrui amesema madaktari bingwa kutoka India wanatarajia kuweka kambi Zanzibar kwa lengo la kuimarisha sekta ya afya nchini.
Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto, Nassor Ahmed Mazrui akipokea zawadi maalum kutoka kwa mjumbe wa Hospital ya Wockhardt ya nchini India, Somnath Shetty alipofika ofisini kwake kujitambulisha.

Ameyasema hayo ofisini kwake Mnazi Mmoja wakati wa hafla fupi ya ujumbe kutoka India uliyofuatana na Mkuu wa Biashara za Kimataifa Somnath Shetty kutoka Wockhardt Hospitals LTD.

Amesema, ujumbe huo unatarajia kushirikiana na Wizara ya Afya kwa kuimarisha huduma za afya kwa jamii pamoja na utoaji huduma za kesi za upasuaji kwa wagonjwa mbalimbali.
Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto, Nassor Ahmed Mazrui akifanya mazungumzo na ujumbe kutoka Hospital ya Wockhardt ya nchini India yenye lengo la kuimarisha sekta ya Afya Zanzibar, mazungumzo hayo yamefanyika huko ofisini kwake Mnazimmoja jijini Zanzibar. (Picha na Fauzi Mussa-Maelezo). Zanzibar). 

Aidha, alisema kesi mbalimbali wanatarajia kuzishughulikia zikiwemo kesi za wagonjwa wanaohitaji kusafirishwa nje ya nchi.

Alisema kuwa, wajumbe hao wanatarajia kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia sekta ya afya kwa ajili ya kutoa huduma za matibabu bora kwa wananchi wake.

Waziri huyo alifurahishwa na ujumbe huo wenye lengo la kuisaidia Zanzibar katika utoaji wa huduma za afya na kueleza fursa hiyo itasaidia kuwajengea uwezo pamoja na ujuzi wa kiutendaji kupitia kwa Madaktari Bingwa kutoka India katika hospitali za Mkoa na Wilaya.
“Serikali imejenga hospitali nyingi za wilaya na mikoa hivyo ni fursa pekee ya kupata wataalamu hao ambao watasaidia kutoa ujuzi kwa wafanyakazi pamoja na kutoa huduma bora kwa wananchi,”alisema Waziri.

Nae Mkuu wa Biashara Kimataifa, Somnath Shetty kutoka Wockhardt Hospitals LTD amesema, lengo la ujio wake ni kuleta ushirikiano wa pamoja katika kuwapatia huduma bora wananchi wa Zanzibar.

Amesema, azma yao hiyo ni kuweka kambi ya Madaktari bingwa hapa Zanzibar kwa kutoa huduma mbalimbali za kiafya ikiwemo za upasuaji wagonjwa wenye kesi ambazo zinahitaji kusafirishwa nje ya nchi.

Akitoa rai kwa wananchi wa Zanzibar amewataka kukata bima ya afya ya kimataifa ili kuwasaidia kupatiwa huduma ya afya ya nje ya nchi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news