NA HUGHES DUGILO
KATIKA kuhakikisha shughuli za Sekta ya Utalii nchini zinarejea na kuendelea baada ya kuathiriwa na janga la UVIKO-19, Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imeendelea kutoa mafunzo kwa watoa huduma za utalii nchini.
Dkt. Naiman Mbise Mratibu wa Mafunzo kwa watoa huduma katika mnyororo wa Sekta ya Utalii akizungumza alipokuwa akitoa hotuba ya utangulizi juu ya Mafunzo hayo.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Utalii Dkt. Shogo Mlozi Akizugumza na waandishi wa habari katika mahojiano maalum mara baada ya kumalizika kwa hafla fupi ya ufuguzi.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo Afisa Mtendaji Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Utalii Dkt Shogo Mlozi Sedoyeka, amesema kuwa, chuo hicho kinaendelea kutoa mafunzo hayo ambayo yamefadhiliwa na MPANGO WA MAENDELEO KWA USTAWI WA TAIFA NA MAPAMBANO DHIDI YA UVIKO-19, kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii na kwamba mafunzo hayo yanatolewa katika mikoa nane ya Tanzania Bara ikiwemo Lindi, Mtwara, Iringa, Mbeya, Ruvuma, Njombe, Mwanza, na Mara.
Dkt.Sedoyeka amesema, lengo la mafunzo hayo ni kuhakikisha wanarudisha shughuli za utalii katika hali yake ya awali na kufikia malengo ya taifa ya kufikia watalii milioni 5 ifikapo mwaka 2025, kwa sababu ya janga la UVIKO-19 liliathiri sana sekta ya utaliI.
Amesema, UVIKO-19 iliathiri kwa kiwango kikubwa Sekta hiyo na watalii kupungua kutoka milioni 1.5 mwaka 2019 hadi 620,000 ambapo serikali kupitia chuo hicho imefanya jitihada mbalimbali ikiwemo ya kutoa mafunzo hayo.
Aidha, amefafanua kuwa serikali ilitoa fedha hizo kwa ajili ya mafunzo hayo ambayo yamelenga kuwajengea uwezo watoa huduma wa Sekta hiyo na kupata uelewa wa namna ya kufanya shughuli zao kwa kufuata miongizo na kuchukua tahadhari katika kukabiliana na janga la UVIKO-19.
Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mkuu wa Wilaya ya Magu Salum Kalli, amesema Sekta ya Utalii imechangia kuongeza fedha za kigeni kwa taifa kwa asilimia 25 na zaidi ya asilimia 17 katika Pato la taifa pia kuchangia ajira milioni 1.6.
Kalli amesema,janga la UVIKO-19 limeathiri sekta ya utalii duniani ambapo kwa hapa nchini imeshuka pia, kuyumba kwa biashara za utalii kwa sasa katika sekta ya utalii nchini imeanza kukamilika.
"Sekta ya utalii ni muhimu katika kukuza pato la taifa,fursa kwenu kualika wawekezaji waweze kuwekeza mkoani Mwanza katika sekta ya utalii kwani tunajukumu la kukuza mji wa Mwanza kwa kutengeneza fukwe ndani ya Ziwa Victoria,"amesema Kalli.