Maghariba 20 wasalimisha zana za kazi

*Zilikuwa zinatumika kukeketa watoto wa kike

NA MARY MARGWE

MAGHARIBA wa jamii ya Kimasai wapato 20 wamesalimisha zana zao maarufu kama shoka (Omorunya) kwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara, Carolina Mthapula zilizokuwa zilkitumika kwa ajili ya kukeketea watoto wa kike wa jamii yao mbele ya maelfu ya watu waliohudhuria Siku ya Maadhimisho ya Wanawake Duniani.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara, Carolina Mthapula akionesha dhana au kifaa kinachotumika kwenye shughuli ya ukeketaji wa watoto wa kike maarufu kama shoka ( Omorunya) aliyokabidhiwa na Mwenyekiti wa kikundi hicho cha Manghariba, Naserian Alais (kulia ) kushoto ni Mkuu wa wilaya hiyo, Dkt.Suleiman Serera.Maghariba hao wamekuwa wakiishi Kjiiji Lobosoiti A Kata ya Emboret wilayani Simanjiro mkoani Manyara. (Picha na Mary Margwe).

Mwenyekiti wa Manghariba hao, Naserian Alais kutoka Kijiji Lobosoiti A Kata ya Emboret wilayani Simanjiro mkoani Manyara alisema wao walikuwa na kikundi chao maarufu kwa jina la Napokie chenye watu wapatao 20 waliokuwa wakijihusisha na vitendo kwa ukatili kwa kuwakeketa watoto wa kike.

Alais alisema, kuacha kuendelea na vitendo hivyo kulitokana na kukalishwa chini na Mkurugenzi wa Shirika la Ushirikishwaji na Uwezeshaji wa Kijinsia ( FPCT ), Elia Ngurumwa na timu yake kuanza kulivalia njuga suala hilo kisha ndipo wakaanza kuwaelimisha juu ya kuachana kabisa na hizo mila potofu za ukatili dhidi ya watoto wa kike.

"Tunaishukuru sana Serikali pamoja na hilo shirika la FPCT kwa kuwa nasi katika kutuelimisha juu ya kuacha kabisa hii mila ya kuwakeketa watoto wetu, na kweli tumefanikisha chini ya Mkurugenzi wa shirika hili Elia Ngurumwa pamoja na timu nzima, hakika wamefanya kazi nzuri sana kwetu, na leo hatimaye tumekabidhi vifaa vyetu ili kuachana kabisa,"alisema Alais.

Aidha, alisema ni vizuri kuwapa watoto wa kike haki zao za msingi kwa kuiwasomesha, kutokufanya hivyo ni kuwanyanyasa watoto wa kike na kuwanyanyasa watoto wasio na hatia, ambapo walikuwa wakifanyiwa ukatili huo kuanzia mtoto alipokua na umri wa mwaka mmoja hadi 18.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara, Carolina Mthapula akiwapongeza baadhi ya Maghariba kati ya 20, mara baada ya kukabidhi vifaa vyao kwenye maadhimisho ya siku ya wanawake duniani iliyofanyika kimkoa wilayani Simanjiro, ambapo mgeni rasmi alikuwa Katibu Tawala huyo, kulia ni mkuu wa wilaya hiyo, Dkt.Suleiman Serera. (Picha na Mary Margwe).

Aidha, alifafanua kuwa ukeketaji umeleta madhara makubwa kwa watoto wa kike, kwa maana akipata mimba na kwenda kujifungua hutokwa na damu nyingi na pengine baadaye hupoteza maisha kabisa.

"Ndio maana tumekaa tumetafakari, sasa tumeamua kuwakeketa watoto wetu wa kike, na ikumbukwe kuwa ndio maana sasa tumesimama na kuelimisha kwamba tumekataa kabisa ukeketaji kwa watoto kwa watoto wetu, sasa tumeona madhara yake, nawaambia wanawake wote wa kimasai tusimame imara kulipinga hili hatutaki tena kuwakeketa watoto wetu,tumeona kufanya hivyo ni kutafuta laana maana tunakuwa tumewafanyia ukatili mkubwa, kikubwa na cha msingi ni kuwapatia elimu,"aliongeza Ngariba huyo.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara, Carolina Mthapula akiwapongeza baadhi ya Maghariba kati ya 20, mara baada ya kukabidhi vifaa vyao kwenye maadhimisho ya siku ya wanawake duniani iliyofanyika kimkoa wilayani Simanjiro, ambapo mgeni rasmi alikuwa Katibu Tawala huyo, kulia ni mkuu wa wilaya hiyo, Dkt.Suleiman Serera. (Picha na Mary Margwe).

Kufuatia hilo, Katibu Tawala wa Mkoa huo Carolina Mthapula alimpongeza mama huyo kwa kitendo walichokitenda cha kukabidhi vifaa kwake na kusema kuwa ni kitendo cha ujasiri na pia ni upendo katika jamii, maana wamethubutu wenyewe baada ya kuelimishwa, na hivyo ameitaka halmashauri ya wilaya hiyo kuhakikisha wanashauriwa kuunda kikundi ili waweze kupatiwa fedha za kuanzisha biashara ili kujikwamua kiuchumi.

Hata hivyo, katibu tawala huyo, aliwataka maghariba hao kuhakikisha sasa wanawekeza nguvu zao katika kuwasomesha watoto wa kike na wa kiume badala ya awali walipokua wakielekeza nguvu nyingine katika kuwaza juu ya ukeketaji wa watoto wa kike, hivyo sasa waone kama vilishapita wafungue ukurasa mpya wa kuwainua watoto kimasomo na kufuafilia maendeleo yao shuleni.

Naye Mkurugenzi wa shirika la Ushirikishwaji na Uwezeshaji wa Kijinsia ( FPCT) Maasai Gender Particition and Empowerment Project Simanjiro), Elia Ngurumwa alisema kikundi hiko kwa sasa tayari wamekubaliana na mabadiliko ya maendeleo, kwani baada kuwasaidia kuwaelimisha na kuelewa waliweza kwenda kwenye ofisi ya kijiji cha Lobosoiti A na kuwaelezea viongozi kuwa kazi ya kukeketa sasa wameiacha kabisa.

Hata hivyo, Ngurumwa aliongeza kuwa baada ya hapo walikuwa wakitembea kila kitongoji kuelezea hilo, kisha kwenda kwenye mikutano ya wanawake na kujielezea kuhusiana na kuachana na hizo mila potofu ya kukeketa watoto wa kike.

"Shirika hili limeanzishwa miaka miwili iliyopiga ikiwa na dhana muhimu za usawa wa jinsia ndani ya jamii, ikiwa na lengo la kupunguza migogoro isiyo ya lazima, haki ya kufikia, kuitumia, kunufaika, na kumiliki rasilimali ya nchi, haki ya kufikia na kufaidi huduma za msingi,"alisema Ngurumwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news