NA MARY MARGWE
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Philip Mpango amefungua Daraja la Magara linalounganisha wilaya za Babati na Mbulu mkoani Manyara.
Dkt.Mpango akizungumza Machi 16, mwaka huu wakati akizindua daraja hilo amesema ni haki ya wananchi kupatiwa huduma baada ya wao kulipa kodi.
Amewaahidi wananchi wa Mkoa wa Manyara, kujengwa kwa barabara za lami zilizoahidiwa kwenye ilani ya uchaguzi wa CCM.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini (TANRODS), Rogatus Mativila amesema daraja hilo limejengwa na kampuni ya China Railway Seventh Group (CRSG) kwa gharama ya shilingi bilioni 12.6.
Mativila amesema daraja hilo lina urefu wa mita 84 na sehemu tatu za mita mbili pembeni na meta 36 katikati na nguzo 70 za kusimika ardhini.
Amesema, wamejenga kalavati kubwa, makalavati madogo 11, mifereji mita 800 na kuweka taa 16 za barabarani.
Mwanafunzi wa kidato cha nne wa Shule ya Sekondari Magara, Amina Omary amesema kukamilika kwa daraja hilo kutawasaidia kupita kipindi cha mvua kubwa zikinyesha.