>Aweka jiwe la msingi mradi wa maji Orkesumet wa Bilioni 41.5/-
NA MARY MARGWE
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Philip Mpango amezindua Wiki ya Maji pamoja na kuweka jiwe la msingi mradi wa maji wa Orkesumet unaogharimu sh.bilioni 41.5 uliopo Simanjiro mkoani Manyara.
Dkt.Mpango ameweka jiwe la msingi mradi huo uliofadhiliwa kwa asilimia 100 na Serikali ya Tanzania ambao umekamilika kwa asilimia 99.
Akizungumza na wananchi wa Loiborsoit mara baada ya kuweka jiwe la msingi katika mradi huo, Makamu wa Rais amewataka wananchi wa eneo hilo kuendelea kulinda mradi huo ikiwa ni pamoja na kutunza mazingira ili kutopoteza chanzo cha maji kilichopo katika eneo hilo kinachotegemewa katika mradi mkubwa wa maji wa Orkesumet.
Amesema, serikali imetumia fedha nyingi sana kugharamia mradi huo, ili wananchi wake waweze kupata huduma ya maji ambayo ni suala muhimu na ndio uhai.
"Hakika mradi huu utawanufaisha wananchi na kuwapunguzia mzigo wanawake waliokuwa wanatumia saa tano kufuata maji kwa punda,"amesema Dkt.Mpango.
Aidha, amesema mradi huo umekuwa ni mkombozi mkubwa kwa wananchi wa Simanjiro, kwani Kwa kipindi chote hawajawahi kupata Maji , hivyo kupata maji kwao ndio kila kitu, kikubwa ni kuhakikisha mradi huo unatunza ili kuja kuwanufaisha vizazi na vizazi.
Kwa upande wake Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema wanawake wa Simanjiro awali walikuwa wakitembea umbali wa kilomita 40 kufuatia Maji, kiasi ambacho kwenda na kurudi ni sawa na kilomita 80, ambapo kwa sasa adha hiyo imebaki kuwa historia.
Aweso amesema wizara itaendelea kutekeleza miradi kwa ufanisi pamoja na kuokoa gharama zisizo za lazima katika utekelezaji wa miradi hiyo.
Waziri Aweso amesema, utekelezwaji wa mradi huo kwa kutumia wakandarasi wa ndani unatoa fursa ya kuaminiwa kwa wakandarasi wa ndani ya nchi huku akiwataka watendaji katika wizara hiyo kufanya kazi kwa bidii ili kuendana na kasi ya Serikali ya Awamu ya Sita.
Aidha, mmoja wa madiwani wa viti maalum wa halmashauri ya wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara humo, Bahati Patison Mosses anaishukuru Serikali ya Awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kuwakumbuka katika kuwapatia mradi huo wa maji ambao kwao ni tunu kubwa.
Hata hivyo, Mosses ameongeza kuwa, mradi huo ni msaada mkubwa kwa jamii ya Simanjiro kwani kwa jamii ya Kimasai wanaotakiwa kutafuta maji ni akina mama, hivyo akina mama hao walikuwa wakilazimika hata kulala siku mbili hadi tatu kukesha kusubiria maji.