Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Nchini (DCEA) yataja mafanikio lukuki kuelekea Mwaka Mmoja wa Uongozi wa Rais Samia madarakani

*Yasema mengi yamefanyika, yaahidi makubwa zaidi

NA GRACE SEMFUKO-MAELEZO

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Nchini (DCEA) katika kipindi cha mwaka mmoja wa uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan madarakani, imedhibiti uingizwaji wa tani 120.5 za kemikali bashirifu aina ya yabisi, pamoja na lita 40 za kemikali hiyo aina ya kimiminika ambazo zilikuwa zikiingizwa nchini.

Mamlaka hiyo katika kipindi hicho pia, iliweza kukamata wafanyabiashara na watumiaji wa dawa za kulevya 11,716 ambao walidaiwa kukutwa na kilo 35, 227. 25 za dawa za aina mbalimbali.
Akitoa taarifa ya mwaka mmoja ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan madarakani, Kamishna Jenerali wa DCEA, Gerald Kusaya, amesema pia wameteketeza ekari 185 za mashamba ya bangi katika maeneo mbalimbali nchini, na mashamba ya mirungi ekari 10 ambapo katika zoezi hilo, wapo watuhumiwa waliofikishwa mahakamani na kesi zao zinaendelea kusikilizwa.

"Katika kipindi hicho jumla ya watuhumiwa 100 walikutwa na dawa aina ya Cocaine, lakini pia katika kipindi hicho watuhumiwa 588 walikamatwa wakiwa wanajihusisha na biashara na utumiaji wa dawa za kulevya aina ya Heroine, watuhumiwa 9,484 walikamatwa wakijihusisha na dawa za kulevya aina ya bangi, watuhumiwa 1,395 walikutwa wafitumia na kufanya biashara ya mirungi, katika kipindi hicho mashamba 132 ya watuhumiwa 132 wa mashamba ya bangi walikamatwa,"amesema.

Kusaya amesema kufuatia Tanzania kufanya vizuri kwenye udhibiti wa kemikali hizo, Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kudhibiti Dawa za Kulevya na Uhalifu-UNODC imeiteua Tanzania kuwa nchi kinara katika udhibiti wa kemikali bashirifu, na kuipa jukumu la kutoa elimu kuhusu udhibiti wake katika nchi tisa barani Afrika.

"Watanzania wenzangu, kutokana na taasisi yenu kufanya vizuri sana kwenye udhibiti wa dawa bashirifu, Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kudhibiti Dawa za Kulevya na Uhalifu-UNODC imeiteua Tanzania kutoa elimu kuhusu udhibiti huo kwa nchi za Rwanda, Burundi, Madagascar, Zambia, Malawi, Ethiopia, Msumbiji, Eritrea na Mauritius," amesema Kusaya.

Aidha, amebainisha kuwa DCEA kwa kushirikiana na taasisi na za Serikali za Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba TMDA, Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Bohari ya Dawa- MSD na Bodi ya Kimataifa ya Kudhibiti Dawa za Kulevya wanasaidiana katika kudhibiti uchepushaji wa kemikali bashirifu, ili kuondokana na dawa za kulevya ambapo wameanzisha mradi wa ushirikiano kati ya Serikali na taasisi 27 za kemikali hiyo, na vyama viwili vya dawa za binadamu, ambapo wametia saini mkataba wa makubaliano ya udhibiti huo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news