*Wapongeza kwa hatua hiyo
NA MWANDISHI DIRAMAKINI
KUFUATIA Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kibaha Mjini kuwa na changamoto ya simu za kusajili wanachama wake kidijitali wa Jimbo la Kibaha Mjini, Silvestry Koka ametoa simu janja 14 kwa kata zote za jimbo hilo.
Akizungumza na viongozi wa sekretarieti za kata kwenye jimbo hilo,Mbunge huyo amesema ameamua kujitolea simu hizo ili zirahisishe usajili wa wanachama wa zamani na wapya kisasa.
Koka amesema kuwa, wakati chama kinaelekea kuchagua viongozi wake lazima itambue wanachama wake kidigitali.
Amesema kuwa, kila kata itapata simu moja ndiyo sababu ameamua kuunga mkono chama kutambua wanachama wake.
Naye mgeni rasmi katika kikao hicho ambaye ni Katibu wa CCM mkoa wa Pwani, Said Goa alisema kuwa simu hizo zitasaidia kwenye usajili wa wanachama.
Goa amesema kuwa, wilaya hiyo ilikuwa ya mwisho kwenye usajili wa wanachama kwa njia hiyo kati ya Wilaya tisa za mkoa huo.
Amesema kuwa, moja ya changamoto walizokuwa nazo ni ukosefu wa simu za kusajilia wanachama.
Naye Diwani wa Viti Maalum, Selina Wilson alisema kuwa msaada huo utasaidia kwani walikuwa na wakati mgumu kujichangisha hadi kununua simu hizo.
Wilson amesema kuwa, watashirikiana na viongozi wa kata ili kusajili wanachama kwenye maeneo yao.
Kwa upande wake mwenyekiti wa CCM Kata ya Kongowe, Simon Mbelwa alisema kuwa watapita mtaa kwa mtaa ili kuwafikia wanachama wote.