*Ni kuhusu kituo cha afya, umeme na suala la shule moja ya bweni ya wasichana katika kila mkoa
NA MARY MARGWE
MBUNGE wa Viti wa Maalum mkoani Manyara, Regina Ndege ameelekeza kero tatu kwa Makamu wa Rais, Dkt.Philip Mpango ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa kituo cha afya Magara kisichokua na dawa pamoja na wahudumu wa afya, na hivyo kupelekea akina mama kufuata huduma ya kujifumgulia mbali na eneo hilo.
Aidha, Ndege anaipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa kazi nzuri inazoendelea kutekelezwa ikiwa ni pamoja na kujenga miundombinu mbalimbali kama shule, madarasa, pamoja na vituo vya afya.
"Kupitia ujio wako huu, tunakuomba Mheshimiwa Makamu wa Rais wewe ni msikivu, ni mpole ni mpenda watu, tunakuomba serikali yako isikie kilio cha eneo hili la hapa, wananchi hawa wapate huduma, madawa yawepo na madaktari waongezwe ili waweze kupata huduma hii kiurahisi zaidi,"aliongeza Mbunge huyo.
Aidha, pia aliipongeza serikali hiyo kwa kuanzisha mpango wa kuwa na umeme katika kila kaya, licha ya kuwa maeneo mengi umeme umefika, lakini bado vijiji vingine vingi havijapata umeme, isipokua yapo maeneo ambayo wananchi wanapata gharama kubwa ya kuingiza umeme badala ya ile ya sh.27,000 yapo maeneo wanaingiza umeme kwa sh.320,000.
Mbali na hilo Mbunge huyo pia ameiomba serikali hiyo kupewa kipaumbele cha kupatiwa shule ya sekondari ya bweni kama ambavyo mkoa huo uko katika mpango huo, hivyo ameomba mkoa huo katika bajeti hiyo ya serikali kupata kipaumbele ili shule hiyo iweze kujengwa katika mpango huo wa mwaka huu.
"Nashukuru serikali yetu ya Awamu ya Sita kwa kuanzisha mpango wa kuwa na shule moja katika mkoa ya bweni ya wasichana, na mkoa wetu uko katika mpango huo wa kupewa shule, lakini kwa kupitia ujio wako huu niendelee kuiomba serikali kwamba kwa kuwa mkoa wetu uko katika ule mpango tunaomba tupewe kipaumbele, kwa sababu jografia ya mkoa huu Mheshimiwa Makamu wa Rais ni ngumu mno,"alisema Ndege.
Aidha aliongeza kuwa, "watoto wetu wa kike wa ni wachache wanaofanikiwa kwenda form five na six, na ni wachache wanaoweza kufika kwenye masomo ya sanyansi kwa sababu wengi wanaishia katika elimu ya ya form four, kwa hiyo kupitia ujio wako tunakuomba Mheshimiwa Makamu wa Rais kwa bajeti hii ya serikali Mkoa wetu wa Manyara tupewe kipaumbele ili shule hii ianze kujemgwa kwenye mpango huu wa mwaka huu,"aliongeza Mbunge.