>Yadhamiria kujikita katika tafiti zinazohusu kazi, ajira, vijana na wenye ulemavu nchini
MWANDISHI MAALUM
OFISI ya Waziri Mkuu- Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu imebainisha mipango mikakati ya kiutendaji katika majukumu inayoyaratibu ili kuhakikisha Maelekezo ya Mhe. Rais na Mhe. Waziri Mkuu yanatekelezwa kwa ufanisi na weledi katika kuboresha huduma za ofisi hiyo, baada ya mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan.
Akieleza mwelekeo wa ofisi hiyo, kwa waandishi wa habari Machi 20,2022 jijini Dar es Salaam, Mhe. Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu),Patrobas Katambi amefafanua kuwa pamoja na kuwa ofisi hiyo imetekeleza kwa mafanikio majukumu yake, hatua inayofuata ni kujikita katika tafiti katika masuala inayoratibu ya Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu.
“Tumeanza kufanya upembuzi katika baadhi ya maeneo, Kwa sasa tatizo la ukosefu wa ajira duniani ni 13.6 kwa mujibu wa UNESCO, ambapo 75% ya Vijana wapo katika ajira ya Sekta isiyo rasmi. Kwa Afrika na Asia 96% ya nguvu kazi ni vijana. Kwa mantiki hiyo tunakusudia kuiwezesha sekta Binafsi kwa kuwa ndiyo inayo ajiri vijana wengi,"amesema Katambi.
Mhe. Katambi amefafanua kuwa, Mhe. Rais amewataka waandae programu maalum ya kutengeneza fursa za Ajira kwa vijana, ambapo programu hiyo itahusisha wizara, idara, wakala na taasisi zote za serikali, Sekta Binafsi.
"Programu hiyo itahakikisha kuwa kila fedha inayotokana na serikali kwa hapa ndani au tunazozipata kutoka nje ya nchi, iweze kuzalisha fursa za ajira kwa vijana waliojiajiri au kutengeneza ajira,”amesisitiza Katambi
Ameongeza kuwa, programu hiyo itajikita pia katika katika miradi mikubwa ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali, ambapo utekezaji wa miradi hiyo utaweza kuzalisha ajira za moja kwa moja na ambazo sio za moja kwa moja.
“Viongozi wetu wameshaanza Mipango mikakati ya mashauriano, vikao vya kikanda na kimataifa katika kufungua na kupanua wigo zaidi wa kutengeneza fursa za kimtaji na ajira. Aidha, Mkakati mwingine ni kuiwezesha Sekta Binafsi kwa kuwa ndiyo inayo ajiri zaidi kwa sekta zisizo rasmi. Pia tunaendelea na kufanya tafiti za mifumo ili kulegeza masharti ya ukopeshaji na riba za kibenki pamoja na taasisi za kimaendeleo,”amesema Katambi.
Amefafanua kuwa, mkakati mwingine ambao ofisi hiyo iliyonao ni kuzitafuta taasisi na wadau wa kimaendeleo watakao weza kutoa ruzuku, misaada pamoja na fedha zitakazo wawezesha vijana kujiajiri.
Aidha, ameongeza kuwa wamejipanga kufanya Ufuatiliaji wa fedha zinazotolewa na halmashauri kwa ajili ya kuwakopesha Wanawake, Vijana na Wenye Ulemavu ambapo hadi sasa, zaidi ya shilingi bilioni 145.8 zimetolewa kote nchini.
“Serikali hii imeelekeza, baada ya kuwawezesha vijana kuweza kukopesheka katika vikundi, lazima 30% ya zabuni zitakazo zinatolewa kwenye Halmashauri wapewe vijana hao, Pia Mafunzo ya Utambuzi na takwimu hii ikiambatana na kuwawezesha kupata mikopo na mifuko yetu ya Hifadhi ya jamii imeshaanza kutekelza hilo,"amesisitiza Katambi.
Aidha, amefafanua kuwa tayari maelekezo yametolewa ili vijana waliopata mafunzo ya uanagenzi taribani 14,134, ambapo serikali ilitumia shilingi bilioni 9 kuwapa mafunzo hayo, hao vijana nao wapewe mikopo katika halmashauri husika ili waweze kujiajiri.