Mheshimiwa Sagini atoa rai matumizi fedha za mfuko wa jimbo

NA FRESHA KINASA

MBUNGE wa Jimbo la Butiama Mkoa wa Mara ambaye ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mheshimiwa Jumanne Sagini, amewataka wenyeviti wa vijiji, maafisa watendaji wa vijiji na kata katika jimbo hilo kusimamia kikamilifu fedha watakazopewa za mfuko wa jimbo katika maeneo yao, ziweze kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa kwa manufaa ya wananchi.
Mheshimiwa Sagini aliyasema hayo Machi 9, 2022, wakati akizungumza na viongozi hao wilayani humo, ambapo alisema jumla ya Shilingi milioni 47.9 za mfuko wa jimbo hilo zimegawanywa katika vijiji na taasisi kutekeleza shughuli mbalimbali za maendeleo, hivyo viongozi hao wana jukumu la kuzisimamia vyema ziweze kutumika kwa ufanisi kuwaletea maendeleo wananchi na si vinginenvyo.

Alisema, miaka ya nyuma fedha za mfuko wa jimbo zilizokuwa zikitolewa kutekeleza shughuli za maendeleo hazikutumika ipasavyo, bali viongozi walishindwa kufanya usimamizi madhubuti kama ilivyokusudiwa, ambapo kwa sasa amesema watakaofanya mchezo na fedha hizo watachukuliwa hatua kali za kisheria bila kufumbiwa macho.

"Uzoefu wa huko nyuma fedha za namna hii ziligawanwa tu, sio kwamba Butiama fedha zilikuwa haziji bali zilikuwa zinakuja miaka yote. Watu waligawana gawana na kulipana posho hakuna kitu kilifanyika cha maana, na mimi kwa kweli sina tamaa ya kula hata shilingi moja lazima fedha hizi ziende kutatua shida za wananchi, watu wamehangaika wamefanya kazi na mimi nimewaambia mkijikuna nitawaunga mkono, lazima wananchi ziwaletee matokeo chanya,"amesema Mheshimiwa Sagini.

"Sasa ninyi Watendaji wa Vijiji, Wenyeviti wa Vijiji na Maafisa Watendaji kata mnajua mchezo ambao huwa mnaufanya na hela za serikali, tumeamua kuwaletea hizi fedha Shilingi Milioni 47.9 jasiri wa kula ale tunataka hizi hela zikiingia ndani ya wiki mbili ndugu viongozi, tamaa yetu sisi chama chenye ilani na Mheshimiwa Rais ambaye ni Mkuu wa Serikali ni kuona hizi fedha zinatatua matatizo ya Wananchi,"amesema Mheshimiwa Sagini.

Aidha, Mheshimiwa Sagini amewataka Watumishi Wilayani humo, kuendelea kufanya kazi kwa weledi na kuhakikisha dhamana waliyopewa kuwatumikia wananchi wanaitumia vyema kwa kujikita zaidi kutatua kero zao katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news