NA MARY MARGWE
MBUNGE wa Viti Maalum wa Mkoa wa Manyara, Yustina Rahhi amekabidhi msaada wa magodoro 30 kwa ajili ya wafungwa waliopo gereza la Wilaya ya Mbulu ili kupunguza changamoto ya upungufu wa magodoro.

Akizungumza wakati akikabidhi magodoro hayo Machi 12, 2022 Rahhi amesema magereza ni chuo cha mafunzo hivyo wafungwa nao wanapaswa kulala sehemu nzuri wakati wakitumikia adhabu.
“Jamii inapaswa kujitoa na kusaidia taasisi mbalimbali zenye uhitaji ikiwemo hospitali, shule, vituo vya watoto yatima na wenye kuishi katika mazingira hatarishi hasa kipindi hiki cha Kwaresma,”amesema Rahhi.


Amesema, ni vyema kutoa misaada kwenye taasisi hizo zenye mahitaji ya kibinadamu kama vile malazi bora, chakula na mavazi ili nao waweze kujisikia vyema kwenye maisha yao.

Kwa upande wake, Mkuu wa magereza wilaya ya Mbulu, Alfonse Katunzi amemshukuru na kumpongeza mbunge huyo kwa kujitolea magodoro 30 kwa ajili ya wafungwa hao wa Gereza la Mbulu.