Mkuu wa Majeshi awasamehe vijana 853 waliofukuzwa katika kambi za JKT kwa makosa ya kinidhamu, aamuru warejeshwe kambini

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

MKUU wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania, Jenerali Venance Mabeyo ametoa msamaha kwa vijana 853 waliofukuzwa katika kambi za JKT Aprili 12, 2021 kutokana na makosa ya kinidhamu.

Hayo yamebainishwa kupitia taarifa iliyotolewa leo Machi 5,2022 na Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano (JWTZ), Luteni Kanali Gaudentius Gervas Ilonda.

Amesema kuwa, CDF Mabeyo ameamuru vijana hao wote warejeshwe katika Makambi ya Kujenga Taifa tayari kwa kuanza mafunzo yao mara moja.

Amesema kuwa, Aprili 12,2021 jumla ya vijana wa Kitanzania 854 ambao walikuwa wanaendelea na mafunzo ya kujitolea kwenye Makambi ya JKT, walifukuzwa na kuondolewa makambini na kurejeshwa majumbani mwao kutokana na sababu za kimakosa ya kinidhamu.

"JWTZ imepokea na ina taarifa kijana mmoja kati ya wale vijana 854 amefariki na walio hai ni vijana 853,"amesema.

Luteni Kanali Ilonda ameeleza kuwa,msamaha ambao Mkuu wa Majeshi, Jenerali Venance Mabeyo ameutoa kwa vijana hao umekuja baada ya JWTZ kufanya uchunguzi wa kina na utafiti na kujiridhisha na kuonesha kuwa vitendo hivyo vya ukiukwaji wa taratibu za kinidhamu walivyifanya ni kwa sababu ya utoto.

"Wengi wao walifanya hivyo kwa kutojitambua, kurubuniwa na wengine walifanya kwa kufuata mkumbo," amesema Luteni Kanali Ilonda

Aidha, Luteni Kanali Ilonda ameongeza kuwa kuna baadhi ya Watanzania walioshiriki kuwarubuni vijana hao na kutoa wito wa kutofanya vitendo hivyo.

"Tuache vijana wapate mafunzo yao ya stadi za maisha ili waje kulitumikia Taifa lao kwa moyo mmoja," Luteni Kanali Gaudentius Gervas Ilonda, Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano (JWTZ) ameeleza kupitia taarifa hiyo.
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania, Jenerali Venance Mabeyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news