NA ROTARY HAULE
BENKI ya NMB imeshiriki uzinduzi wa Wiki ya Wanawake iliyofanyika Kibaha mkoani Pwani kwa kutambulisha bidhaa mpya mahususi kwa ajili kuwawezesha Wanawake wajasiriamali.
Meneja Mahusiano wa NMB Kitengo cha Biashara na Huduma za Serikali kwa upande wa Dar es Salaam,Pwani na Zanzibar, Irene Masaki amesema lengo la bidhaa hizo ni kuwakwamua wanawake nchini.
Masaki amesema,NMB imekuja na bidhaa ya Jasiri Pamoja,Jasiri Fanikiwa,na Jasiri Bonus ambapo zote kwa pamoja zimeanzishwa kwa ajili ya kuwasaidia wanawake kote nchini.
Amesema,endapo wanawake wakizitumia zitawanyanyua katika shughuli zao na hivyo kukua kiuchumi hali ambayo itawezesha familia zao kuishi maisha bora.
Aidha,Masaki amesema mbali na bidhaa hizo lakini pia hivi karibuni benki hiyo imezindua Jasiri Bond kwa ajili ya watu mbalimbali wakiwemo wanawake.
Amesema, ,Jasiri Bond ni hati fungani ambayo inawaalika watu mbalimbali pamoja na kampuni kuwekeza kwa ajili ya kukopesha wanawake kwa gharama nafuu.
Amesema kuwa,kampuni yoyote au mtu yeyote atakayewekeza katika mfumo wa Jasiri Bond,atapata faida kubwa ya mapato ya asilimia 8.5.
"NMB tumekuja na bidhaa rahisi na nafuu kwa ajili ya wanawake wote nchini ambazo wakizitumia zitawasaidia kujiimarisha kiuchumi kupitia biashara zao wanazofanya,"amesema Masaki.
Masaki amewataka wanawake na wananchi wote kiujumla kuhakikisha wanajitokeza kwa wingi katika benki hiyo kwa ajili ya kuchangamkia fursa hizo kwakuwa benki hiyo imeanzishwa kwa ajili hiyo.
Aidha,ameongeza kuwa kufuatia uzinduzi wa Siku ya Wanawake Mkoa wa Pwani NMB itakuwa katika viwanja hivyo kwa ajili ya kuendelea kutoa elimu ya ujasiriamali kwa wanawake hao.
Amesema,elimu hiyo itakwenda sambamba na kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa kutumia bidhaa hizo ambapo elimu hiyo pia itakwenda nchi nzima.
"NMB tumeshiriki uzinduzi wa Wiki ya Wanawake Mkoa wa Pwani na sisi tutakuwepo hapa wiki nzima kwa ajili ya kutoa elimu ya ujasiriamali kwa Wanawake na kutambulisha fursa zetu zenye riba nafuu ,"amesema Masaki.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge akizindua Wiki ya Wanawake leo Mjini Kibaha amepongeza juhudi zinazofanywa na benki hiyo.
Kunenge amesema kuwa, kutokana na umuhimu huo NMB wanapaswa kuendelea kuzitangaza bidhaa zao ili ziweze kunufaisha wananchi wengi zaidi nchini.
Hata hivyo, Kunenge amesema Mkoa wa Pwani utaendelea kushirikiana na benki ya NMB katika kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo huku akiomba jamii kutumia benki hiyo.