Nyumbu Kibaha lajivunia mafanikio makubwa ndani ya mwaka mmoja wa Rais Samia

NA ROTARY HAULE

SHIRIKA la Tanzania Automotive Technology Centre (TATC) maarufu kwa jina la Nyumbu Kibaha limesema katika kipindi cha mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan limepata mafanikio makubwa.
Mkurugenzi wa uzalishaji wa TATC, Meja Simon Rwegoshora akiwaonesha waandishi wa habari (hawapo pichani) gari la kivita na magari mengine yanayotengenezwa katika shirika hilo.

Miongoni mwa mafanikio hayo ni pamoja na kuanzisha miradi mbalimbali ya utengenezaji wa mashine za kuchakata katani,kufyatua tofali,mtambo wa kutengeneza nyuzi za fedha,mradi wa mashine za kutengeneza taka,na vipuri mbalimbali.

Mafanikio mengine ni kuanzisha mradi wa kutengeneza nguzo za chuma zisizopata kutu kwa ajili ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na vifaa vingine na kwamba kufanya hivyo ni kuunga mkono Serikali ya Awamu ya Sita ya kuanzisha viwanda mbalimbali.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la TATC na Kamanda wa Kikosi cha Nyumbu Project, Hashimu Komba.

Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo ambaye pia ni Kamanda wa Kikosi cha Miradi ya Nyumbu (Nyumbu Project), Brigedia Jenerali Hashimu Komba ametoa kauli hiyo wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari leo Machi 7, 2022 katika ofisi za Nyumbu zilizopo Mjini Kibaha.

Komba amezungumza na waandishi wa habari ikiwa ni sehemu ya kueleza mafanikio ya shirika hilo katika kipindi cha mwaka mmoja cha Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia.

Komba amesema, Shirika la Nyumbu lilianzishwa mwaka 1977 kwa maono ya Rais wa Awamu ya Kwanza, Hayati Mwalimu Julius Kambarahe Nyerere kwa malengo ya kufanya tafiti mbalimbali za kiteknolojia.

Amesema,pamoja na uanzishwaji wake miaka hiyo, lakini katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita ndani ya mwaka mmoja wa Rais Samia shirika limekuwa na mafanikio makubwa.

Komba amesema kuwa, Rais Samia amekuwa wa mfano na kwamba katika kipindi cha mwaka 2021/2022 shirika limepewa shilingi bilioni 9 kwa ajili ya kuendeshea shughuli zake.

Amesema,upatikanaji wa fedha hizo zimetokana na juhudi za Rais Samia kupitisha waraka na mpango wa kuimarisha Shirika wa mwaka 2021/22 na 2030/31 ulioandaliwa na shirika hilo.
Waandishi wa habari wakioneshwa aina ya vipuri vinavyotengenezwa na Nyumbu Kibaha.

"Tunamshukuru Rais Samia kwa kupitisha mpango wetu na ameonesha nia ya kutusaidia na tayari ameagiza fedha zipitishwe na mpaka sasa tayari tumepata shilingi bilioni tisa,"amesema Komba

Komba amesema kuwa, waliandaa waraka huo ikiwa ni mkakati maalum wa kukabiliana na changamoto mbalimbali ikiwemo uchakavu wa majengo pamoja na upungufu wa miundombinu,na ukata wa fedha .

Aidha,amesema kuwa kwa sasa shirika lina imani na Rais Samia kwa kuwa tayari ameonesha nia huku akisema bajeti ya shirika kwa mwaka ni shilingi bilioni 25.
"Bajeti yetu kwa mwaka ni shilingi bilioni 25, lakini tunamshukuru Rais kwa kuwa mwaka huu wa fedha tumepewa shilingi bilioni 9, lakini tunatumia vizuri tulichopata kuanzisha miradi ambayo itasaidia kuimarisha shirika hili,"amesema Komba.

Komba amesema kuwa, mikakati ya Shirika la Nyumbu kwa sasa ni kupanua huduma zake kwa kuanzisha programu mbalimbali ikiwemo ya kuzalisha magari mengi ya zimamoto na magari mengine ya kibiashara.

Mkakati mwingine ni kuanzisha karakana kubwa ya kuunda vipuri vya magari,zana za kilimo na vifaa,kuzalisha wataalamu, kuboresha kitengo cha masoko, kuongeza na kuimarisha teknolojia,pamoja na kutekeleza miradi mama itakayoibuliwa na Serikali.

Aidha,Komba ameiomba Serikali kuendelea kutoa fedha za maendeleo ili ziweze kusaidia katika kuimarisha shirika ambalo lina manufaa makubwa kwa Watanzania na Taifa kwa ujumla.
Awali kabla ya Komba kuzungumza waandishi hao walifanya ziara katika karakana mbalimbali katika shirika hilo, ziara ambayo iliongozwa na mkurugenzi wa uzalishaji wa TATC, Meja Simon Rwegoshora.

Kwa upande wake msemaji Mkuu wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Luteni Kanali Josephat Musila amesema ziara hiyo ni muhimu kwa ajili ya kueleza namna Nyumbu ilivyokuwa na manufaa hapa nchini.

Musila amesema kuwa,katika kipindi cha mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Sita Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa liliona sehemu pekee ya kutembelea ni Shirika la Nyumbu kutokana na umuhimu wake mkubwa.
Hatahivyo,Musila ametumia nafasi hiyo kuwaomba waandishi wa habari waliokuwa katika ziara hiyo kutumia kalamu zaidi kueleza kwa Watanzania kazi zinazofanywa na Shirika la Nyumbu kwa ajili ya faida ya Taifa na jamii kwa ujumla.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news