OPEC Fund kuendelea kuunga mkono miradi ya maendeleo Zanzibar, Rais Dkt.Mwinyi apongeza

*Washirikishwa namna ambavyo Serikali imekusudia kuyafikia matokeo ya haraka kupitia Uchumi wa Buluu
 
NA MWANDISHI DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameupongeza utayari wa Mfuko wa Nchi zinazozalisha Mafuta kwa wingi Duniani (OPEC Fund) wa kuendela kuiunga mkono Zanzibar katika miradi mbalimbali ya maendeleo.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo Machi 30,2022 Ikulu jijini Zanzibar wakati alipokutana na Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Nchi zinazozalisha Mafuta kwa wingi Duniani (OPEC Fund), Alkhalifa Abdulhamid Saleh akiwa amefuatana na ujumbe wake.

Katika mazungumzo hayo, Rais Dkt.Mwinyi amesema kuwa, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inathamini juhudi kubwa zinazochukuliwa na OPEC katika kuiunga mkono Zanzibar ikiwa ni pamoja na kusaidia katika kuimarisha miundombinu ya barabara, elimu na mengineyo.

Hata hivyo, Rais Dkt. Mwinyi alitumia fursa hiyo kumueleza Mkurugenzi huyo azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuimarisha uchumi wake kupitia Uchumi wa Buluu na kumueleza jinsi mikakati iliyowekwa na Serikali anayoiongoza katika kufikia azma hiyo.

Pamoja na hayo, Rais Dkt. Mwinyi alimueleza kiongozi huyo kwamba katika Uchumi huo wa Buluu suala la miundombinu nalo limepewa kipaumbele hivyo, ni matarajio yake kwamba mfuko huo utaendeleza utamaduni wake wa kuiunga mkono Zanzibar ili malengo yaliyokusudiwa katika uchumi huo pamoja na kuibua nyanja nyengine za mashirikiano ikiwemo sekta ya afya.

Sambamba na hayo, Rais Dkt. Mwinyi alieleza haja kwa mfuko huo kuunga mkono juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuviimarisha vyuo vya Amali ili kuwasaidia vijana walioshindwa kuendelea na masomo ya ngazi za juu.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akiongozana na mgeni wake Mkurugenzi wa Opec Fund, Dkt.Abdulhamid Al Khalifa (kulia kwa Rais) baada ya kumaliza mazungumzo yao yaliofanyika katika ukumbi wa Ikulu jijini Zanzibar, Machi 30,2022.(Picha na Ikulu).

Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Nchi zinazozalisha Mafuta kwa wingi Duniani (OPEC Fund), Alkhalifa Abdulhamid Saleh alimuhakikishia Rais Dkt. Mwinyi kwamba,mfuko huo una historia ya kuiunga mkono Zanzibar kwa muda mrefu katika kuimarisha miradi mbalimbali ya maendeleo hivyo, atahakikisha hilo linaendelezwa.

Aidha, Mkurugenzi huyo alimueleza Rais Dkt.Mwinyi kwamba kwa vile mfuko huo una uzoefu na umekuwa ukisaidia vyuo vya amali na kutolea mfano katika nchi ya China hivyo, alimuhakikishia kwamba mfuko huo utaangalia utaratibu wa kuisaidia na Zanzibar.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news