*Ni kuhusu upatikanaji wa taarifa sahihi za wanafunzi walioacha shule kwa sababu mbalimbali ili waweze kurudi darasani
NA ASILA TWAHA,OR-TAMISEMI
NAIBU Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Elimu), Mhe. David Silinde amewataka Maafisa Elimu Watu Wazima wa Mikoa na Halmashauri kusimamia upatikanaji wa taarifa sahihi za wanafunzi walioacha shule kwa sababu mbalimbali ili waweze kurudi shuleni.

Mhe. Silinde amewataka wasimamizi wa elimu ya watu wazima kufanya kazi kwa weledi ili nafasi iliyotolewa na Serikali kwa wanafunzi walioacha shule kwa sababu mbalimbali waweze kurudi shule kuendelea na masomo.

“Haya ni sababu ya usimamizi mzuri wa elimu ya Awali, Msingi Sekondari na Elimu ya Watu Wazima na Elimu Nje ya Mfumo rasmi,”amesema Silinde
Aidha, kuwepo kwa Mpango wa Uwiano kati ya Elimu na Jamii (MUKEJA) na Mpango wa Elimu ya Msingi kwa Watoto Walioikosa (MEMKWA) Mhe. Silinde amesema, Serikali inatambua umuhimu wa elimu ya watu wazima na nje ya mfumo rasmi kupitia Sera ya Elimu ya mwaka 2014 tamko namba 3.3.3.

Amefafanua kuwa, Serikali inaendelea kuboresha mazingira mazuri ya kufundishia na kujifunzia ili kupata idadi kamili ya walengwa wa elimu ya watu wazima na nje ya mfumo rasmi, "ninawaelekeza fuatilieni upatikanaji sahihi wa takwimu za elimu ya watu wazima na nje ya mfumo rasmi kwa kuendelea kuutumia mfumo wa BEMIS,"amesema.
Kwa upande wa Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Elimu), Gerald Mweli amewataka viongozi hao kuendelea kusimamia na kufuatilia wanafunzi wote walioacha shule kwa sababu mbalimbali amesema mpaka sasa takwimu zinaonesha zaidi ya wanafunzi 909 wamesharudi shule kuendelea na masomo kati ya hao wapo wenye sababu mbalimbali zikiwemo utoro na ujauzito.

Aidha, Mhe. Silinde amewaelekeza Wakurugenzi wa Halmshauri zote kutenga bajeti ya kutosha kwa ajili ya elimu ya watu wazima na elimu nje ya mfumo rasmi na kuzisimamia utekelezaji wake.
Naye Martha Ignatus (Afisa Elimu Watu Wazima) ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuboresha mazingira ya watumishi na kuahidi maelekezo yote wanaenda kuyafanyia kazi na kuahidi upatikanaji sahihi wa takwimu.