Polisi wataja majina ya waliofariki katika ajali ya Fuso, majeruhi wilayani Handeni

*Kamanda amewataja watu waliofariki kuwa Juma Mustafa Mohamed mkazi wa Handeni, Mwajuma Hatibu mkazi wa Handeni, Jumanne Adam mkazi wa Soni, Mohamed Said Makakala mkazi wa Handeni mjini, Zaina Ramadhani mkazi wa Handeni Kwa mkono, huku mtu wa sita akiwa bado hajajulikana jina lake

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

WAFANYABIASHARA sita waliokuwa wakiwahi gulio wilayani Handeni mkoani Tanga wamefariki dunia papo hapo na wengine 7sabakujeruhiwa vibaya baada ya gari aina ya Fuso walilokuwa wakisafiria kuacha njia alfajiri ya leo na kupinduka katika korongo katika barabara ya Soni-Mombo wilayani Lushoto mkoani Tanga.
Ajali hiyo imehusisha Fuso hiyo yenye namba za usajili T 239 AFD lililokuwa limebeba watu pamoja na bidhaa zao kama nyanya, vitunguu, kabeji, matunda na nyombo vya nyumbani ambapo lilipinduka baada ya kufeli breki.

Mashuhuda wa ajali hiyo iliyothibitishwa na Kamanda wa Polisi mkoani Tanga, ACP Safia Jongo wanasema Fuso lilishindwa kupunguza mwendo kwenye mteremko mkali wa eneo la Kijiji Cha Nyasa baada ya breki zake kufeli na hivyo kutumbukia kwenye korongo lenye mteremko mkali kwa chini kiasi cha mita 150.

Akizungumza kwa simu kutokea kwenye eneo la ajali Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, ACP Safia Jongo amesema taarifa za awali zilionesha watu wanne ndio waliopoteza maisha papo hapo kwenye ajali na baadaye watu wengine wawili walifariki wakikimbizwa kituo cha afya kilichopo Mombo wilayani Korogwe.

"Waliotutoka mwanzoni tukipata taarifa, walikuwa wanne, wakaongezeka majeruhi wawili na jumla kufikia sita ambapo kati yao waliofariki wanaume ni wanne na wanawake ni wawili,"amesema Kamanda Jongo.

Kamanda amewataja watu waliofariki kuwa Juma Mustafa Mohamed mkazi wa Handeni, Mwajuma Hatibu mkazi wa Handeni, Jumanne Adam mkazi wa Soni, Mohamed Said Makakala mkazi wa Handeni mjini, Zaina Ramadhani mkazi wa Handeni Kwa mkono, huku mtu wa sita akiwa bado hajajulikana jina lake.

Amewataja majeruhi katika ajali hiyo kuwa ni Rumisha Zuberi Msagati mkazi wa Bumbuli wena, Rasuli Said Makalala mkazi wa Handeni Komwale, Mussa Enock Kajia mkazi wa Lukozi mjini, Amina Zuberi Mhina mkazi wa Handeni, Mwajabu Mrisho Mpulizi mkazi wa Handeni Chogo na Mama Latifa mkazi wa Handeni.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news