NA MWANDISHI DIRAMAKINI
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema kwamba ili kuweza kutekeleza mipango ya maendeleo kwa ufanisi katika sekta za viwanda, utalii, ujenzi wa miundombinu na kutoa huduma bora za afya na elimu ni lazima kuwepo na huduma ya maji safi na salama ya uhakika.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akihutubia na kuufungua Mkutano Mkuu wa Uwekezaji wa Sekta ya Maji Barani Afrika uliofanyika Zanzibar katika ukumbi wa Hoteli ya Melia Mkoa wa Kaskazini Unguja leo Machi 11,2022. Uliowashirikisha wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya Tanzania.(Picha na Ikulu).
Rais Dkt. Mwinyi aliyasema hayo leo Machi 11, 2022 wakati akifungua mkutano wa Wadau wa Ngazi ya Juu wa Mashirikiano katika Uwekezaji wa Sekta ya Maji Kusini mwa Afrika (GWPSA), uliofanyika katika Hoteli ya Melia, Kiwengwa, Mkoa wa Kaskazini Unguja ukiongozwa na Mwenyekiti wake Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete.
Katika maelezo yake, Rais Dkt.Mwinyi alisema kuwa, anaamini kwamba mkutano huo utatoa elimu na uzoefu kutoka kwa wataalamu mbali mbali waliojumuika pamoja ili Zanzibar nayo iweze kuimarisha upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi.
Amesema kuwa,mkutano huo pia umekuja wakati muafaka ambapo kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa sehemu nyingi za ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini kumekuwa na changamoto kubwa ya upungufu wa maji.
Rais Dkt. Mwinyi alisema kuwa, amekuwa akijiuliza siku masuala mengi kuhusu mbinu na njia bora za kufanya ili kuweza kuondokana na changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama hapa Zanzibar ambayo bado inawakumba wananchi katika maeneo mbali mbali Unguja na Pemba.
“Kwa hapa Zanzibar nimekuwa nikipokea taarifa za kuendelea kukauka visima mbali mbali vinavyotumiwa na wananchi,”alisema Dkt.Mwinyi.
Aidha, alieleza kufarijika kwake na ufunguzi wa mkutano huo ulioambatana na uzinduzi wa Mpango wa Miaka mitano ya uwekezaji katika sekta ya Maji Zanzibar, ambapo utekelezaji wake utafanywa baina ya kipindi cha mwaka 2022 hadi 2027.
Alieleza matumaini yake kwamba maazimio yatakayopitishwa katika mkutano huo yatakuwa na mchango mkubwa katika kufanikisha malengo ya kuanzishwa Programu hiyo pamoja na kuzitafutia ufumbuzi changamoto mbalimbali zilizopo katika sekta ya maji.
Rais Dkt.Mwinyi alitoa pongezi kwa Mwenyekiti wa Ushirikiano wa Maji Duniani (GWP) Kusini mwa Afrika, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuridhia mkutano huo kuja kufanyika hapa Tanzania.
Pamoja na hayo, Rais Dkt.Mwinyi alisema kuwa, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kufanya juhudi mbalimbali za kuimarisha sekta ya maji hapa Zanzibar ili kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma za maji safi na salama kwa uhakika.
Alieleza mategemeo yake kwamba mkutano huo utatoa fursa ya kujifunza kutoka kwa walioshiriki namna bora ya kuimarisha upatikanaji wa huduma za maji safi na salama pamoja na njia bora za upatikanaji wa uwezeshaji katika sekta hiyo kutoka katika vyanzo vya Kitaifa na Kimataifa ikiwemo sekta binafsi.
Sambamba na hayo, Rais Dkt.Mwinyi alieleza namna Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilivyoweka mikakati yake katika kuimarisha Uchumi wa Buluu ambao ndio Dira ya uchumi wa Zanzibar hivi sasa pamoja na kueleza sekta zilizomo ndani yake.
Alieleza kwamba mikutano ya Taasisi ya Ushirikiano ya Maji Kusini mwa Afrika (GWPS) ambao hufanyika kila baada ya miaka miwili kwa lengo la kufahamu mafanikio yaliyopatikana katika kuimarisha sekta ya maji kwa nchi wanachama pamoja na changamoto zilizopo katika kuimarisha sekta ya maji.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akionesha Kitabu cha Mpango wa Miaka Mitano ya Uwekezaji katika Sekta ya Maji Zanzibar, baada ya kuzindua mpango huo, wakati ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Uwekezaji wa Sekta ya Maji Barani Afrika, uliofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Melia Kiwengwa na (kulia kwa Rais) Rais Mstaafu wa Tanzania Mwenyekiti wa Taasisi ya (GWPSA), Mhe.Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete na (kushoto kwa Rais) Waziri wa Maji,Nishati na Madini Zanzibar, Mhe.Shaib Hassan Kaduara.(Picha na Ikulu).
Amesema kwamba, lengo la mkutano huo ni kupanga na kujadili mbinu mbalimbali za kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa na tabia nchi ili kuimarisha upatikanaji wa maji safi na salama pamoja na kuyaweka mazingira katika hali ya ubora zaidi.
Mapema Rais mstaafu wa Awamu ya Nne wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ambae pia ni Mwenyekiti wa Mkutano huo,Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, alisema kwamba kwa kiasi kikubwa changamoto ya maji katika bara la Afrika husabanishwa na mabadililo ya tabia ya nchi.
Alisema ili kuondokana na tatizo hilo ni lazima miradi mikubwa ya maji itekelezwe kwa haraka ili kukabiliana na changamoto hiyo katika nchi za Afrika.
Aidha, alisema wana programu ambayo imepitishwa katika mkutano wa 34 wa Afrika na upo mfumo uliotengenezwa ili kufikia malengo ya uanzishwaji wa program ya maji Afrika.
Alisema kuwa, lazima viongozi wa nchi za Afrika wawe na mkakati wa pamoja kutoa kipaumbele kuongeza kasi ya upatikanaji wa maji katika mataifa yao.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi na (kulia kwa Rais) Rais Mstaafu wa Tanzania na Mwenyekiti wa Taasisi ya (GWPSA), Mhe.Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete na (kushoto kwa Rais) Waziri wa Maji,Nishati na Madini Zanzibar Mhe. Shaib Hassan Kaduara, wakifuatilia mada ikiwasilishwa wakati wa mkutano huo Mkuu wa Uwekezaji wa Sekta ya Maji Barani Afrika uliofanyika Zanzibar katika ukumbi wa Hoteli ya Melia Kiwengwa Mkoa wa Kaskazini Unguja leo.(Picha na Ikulu).
Mwenyekiti huyo alimuhakikishia Rais Dkt.Mwinyi kwamba taasisi hiyo anayoiongoza itaendelea kuziunga mkono juhudi za Rais Dkt.Miwnyi katika kuhakikisha changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji inapatiwa ufumbuzi hapa Zanzibar.
"Nchi za Afrika lazima ziweke mazingira mazuri ya uwekezaji ili kuvutia sekta binafsi kuwekeza zaidi kwenye maji, jambo litakalosaidia kuondoa hadha ya huduma hii muhimu kwa ustawi wa wananchi,"alisema.
Naye Mkurugenzi Mkuu Mtendaji wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Afrika, Ibrahim Assane Mayaki, akizungumza kwa njia ya mtandao, alisema kuna mahitaji makubwa ya kuleta mabadiliko katika nchi za Afrika katika sekta ya maji.
Alisisitiza mashirikiano kwa nchi za Afrika katika kulenga kutekeleza matarajio ya watu wa Afrika sambamba na kulinda vianzio vyake vya maji ili kuona wananchi wanapata huduma hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Ayoub Mohammed Mahmoud, alisema hali ya ubatikanaji wa maji katika mkoa inaridhisha kiasi lakini bado wananchi wana uhitaji wa huduma hiyo hivyo ni vyema kwa wataalamu kuwa na mazingatio ya upatikanaji wa huduma hiyo lakini pia juu ya kuitunza rasimali hiyo kwa manufaa ya nchi.
Nao viongozi wa Mashirika ya Kimataifa yakiwemo ya Umoja wa Mataifa wakizungumza kwa njia ya mtandao walieleza umuhimu wa sekta ya maji na kueleza namna watakavyounga mkono juhudi zitakazochukuliwa katika kuhakikisha huduma hiyo inapatikana katika .
Katika mkutano huo Rais Dkt. Mwinyi alizindua Mpango wa Miaka Mitano ya Uwekezaji katika Sekta ya Maji Zanzibar pamoja na kutoa tunzo maalum kwa wafadhili wa mkutano huo.