NA MWANDISHI DIRAMAKINI
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, DkT. Hussein Ali Mwinyi ametuma salamu za pole kwa wananchi waliopatwa na maafa kufuatia upepo mkali uliotokea huko katika vijiji vya Kendwa na Nungwi Shehia ya Kiungani katika Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Rais Dkt. Mwinyi ametoa salamu za pole kwa niaba yake, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na wananchi wote anatoa mkono wa pole kufuatia tukio hilo lililowakumba wananchi hao.
Katika salamu hizo, Dkt. Mwinyi amesema kuwa, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar iliyopo katika Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais itafanya tathmini ya tukio hilo ili iweze kujua hasara halisi iliyojitokeza ili kuweza kuwafariji wananchi waliofikwa na maafa hayo.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Ayoub Mohammed Mahmoud upepo mkali ulitokea katika vijiji vya Kendwa na Nungwi Shehia ya Kiungani, Mkoa wa Kaskazini Unguja na kusababisha maafa kwa nyumba zipatazo 36.
Sambamba na uharibifu katika sehemu za majengo ya hoteli tatu za Kitalii huko kwenye mkoa huo ambapo hakuna mwananchi aliyefariki kutokana na tukio hilo.
Rais Dk. Mwinyi amewasihi na kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu wananchi wote waliopatwa na maafa hayo kuwa na subira katika kipindi hiki kigumu.