Rais Dkt.Mwinyi: Sensa ya Watu na Makazi 2022 ni jambo la heri sana, tusonge mbele

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameeleza matumaini yake makubwa kwamba zoezi la Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka huu wa 2022 litakwenda vizuri kutokana na matayarisho mazuri yaliyofanyika ikiwa ni pamoja na kufanikiwa kwa Sensa ya Majaribio.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo Machi 2, 2022 wakati alipokutana na Kamisaa wa Sensa Zanzibar, Balozi Mohamed Haji Hamza akiwa na ujumbe wake Ikulu jijini Zanzibar wakati alipofika kwa ajili ya kutoa taarifa juu ya Sensa ya Majaribio iliyofanyika pamoja na muendelezo wa matayarisho ya zoezi hilo linalotarajiwa kufanyika mwezi Agosti, mwaka huu.

Katika maelezo yake Rais Dkt. Mwinyi amesema kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ipo tayari kuendelea kuunga mkono jitihada hizo na kusisitiza kwamba zoezi hilo kwa vile lina maslahi mapana ya Taifa na wananchi wake, Serikali itaendelea kuliunga mkono wakati wote.

Rais Dkt. Mwinyi amepongeza utaratibu uliwekwa wa ajira kwa watendaji wa zoezi hilo kwani mfumo huo utaondosha malalamiko yaliyowahi kutokea hapo siku za nyuma sambamba na kuweza kupata ufanisi mkubwa kutokana na watendaji ambao watatoka katika maeneo husika.

Amesema kwamba, kutokana na utaratibu huo ana matumaini makubwa kuwa hakutokuwa na eneo ambalo watapatikana watu ambao hawatokuwa na sifa za kufanya kazi hiyo ambayo ina umuhimu mkubwa katika maendeleo ya nchi.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt.Hussein Ali Mwinyi akimsikiliza Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi Zanzibar, Mhe. Balozi Mohammed Hamza, alipofika Ikulu jijini Zanzibar kwa mazungumza na kuwasilisha taarifa ya matayarisho ya Sensa ya Watu na Makazi Tanzania inayotarajiwa kufanyika mwezi Agosti 2022. (Picha na Ikulu).

Mapema Kamisaa wa Sensa Zanzibar, Balozi Mohamed Haji Hamza alitoa pongezi kwa Rais Dkt.Mwinyi kwa miongozo na maelekezo anayotoa juu ya matayarisho ya Sensa ya Watu na Makazi ya Agosti mwaka huu 2022, na kueleza kwamba sensa ya majaribio imefanyika kwa ustadi mkubwa na kuleta matokeo mazuri.

Amesema kuwa, matokeo ya Sensa ya Majaribio ni mazuri kwani zoezi hilo limefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika maeneo yote yaliyochaguliwa kufanyika na kuwashukuru wananchi kwa ushirikiano makubwa waliyoonesha katika maeneo yote ya majaribio Unguja na Pemba.

Amesema kuwa, zoezi la kutenga maeneo ya kuhesabia watu kwa Zanzibar limekamilika kwa asilimia 100 ambapo kwa upande wa Tanzania Bara zoezi hilo kwa sasa linaendelea katika Mkoa wa Dar es Salaam na kumalizikia Mkoa wa Dodoma ambapo linatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi huu wa Machi.

Amesema kuwa, matokeo ya Sensa ya Majaribio hutumika kwa matumizi ya ndani ambayo huwa ni kigezo kinachotumika kupima nyenzo zote za utekelezaji wa zoezi la Sensa pamoja na kuzifanya kazi changamoto zilizoonekana ili kuhakikisha zoezi hilo ifikapo Agosti 2022 linafanikiwa.

Balozi Hamza ametumia fursa hiyo kutoa shukurani kwa Rais Dkt.Mwinyi pamoja na viongozi wengine wote wakuu wa Serikali kwa kufanya uhamasishaji mkubwa wa zoezi la Sensa ikiwa ni pamoja na kuzitumia hotuba zao wanazozitoa kwa wananchi.

Amesema kuwa, tayari wameshakutana na Mawaziri wa Wizara zote hapa Zanzibar kuwapa mukhtasari wa zoezi hilo na kuwaomba watumie nafasi zao katika kila mikutano wanayoifanya kwa azma ya kuwafikishia ujumbe wananchi.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi , Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na kubadilisha mawazo na Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi Zanzibar, Mhe.Balozi Mohammed Hamza wakiwa nje ya ukumbi baada ya kumaliza mazungumzo yao yaliofanyika katika ukumbi wa Ikulu Zanzibar.(Picha na Ikulu).

Ameeleza kwamba taasisi zote za Serikali zikiwemo mikoa na wilaya zimeshakabidhiwa majukumu ya utendaji kuhusu kuhamasiha zoezi hilo la Sensa huku akipongeza mashirikiano wanayopata kutoka ngazi ya Taifa hadi katika uongozi wa Masheha.

Aidha, Balozi Hamza alieleza mipango iliyowekwa katika kuhakikisha suala la ajira linafanyika ipasavyo kwa kuwaajiri makarani wa Sensa pamoja na wasimamizi maudhui ambapo zoezi hilo linatarajiwa kuanza mwezi wa Aprili na litahushisha Wakuu wa Mikoa na Wilaya ambapo waajiriwa hao watatoka katika Shehia zao ili kurahisisha utekelezaji wa zoezi hilo.

Nae Kaimu Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mashavu Khamis Omar alieleza namna ya zoezi hilo litakavyofanyika siku itakapofika kwani kila mwananchi atahesabiwa katika eneo husika alilolala na hapatotokea mtu kuhesabiwa mara mbili hiyo ni kutokana na teknolojia itakayotumika.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news