*Wananchi wamshukuru kwa juhudi zake za kuhakikisha wanapata maji safi na salama
NA MWANDISHI DIRAMAKINI
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa kwa vile maji ni uhai lazima Serikali iongeze kasi ya upatikanaji wa huduma hiyo kwa wananchi kwa kuendeleza na kuanzisha miradi mipya ya maji safi na salama.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akiwasili katika viwanja vya ujenzi wa Mradi wa Matenki ya Maji Safi na Salama Kwarara Kidutani Wilaya ya Magharibi “B” Unguja, wakati wa Uwekaji wa Jiwe la Msingi Mradi wa Uhuishaji na Uimarishaji wa Mfumo wa Usambazaji Maji Zanzibar ikiwa ni Wiki ya Maji Duniani,kulia kwa Rais ni Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Mhe. Idrisa Kitwana Mustafa, Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Zena Ahmed Said na Spika wa Baraza la Wawakilishi, Mhe.Zuberi Ali Maulid.(Picha na Ikulu).
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la Mradi mkubwa wa Uhuishaji na Uimarishaji wa Mfumo wa Maji Safi na Salama, huko Kwarara Kidutani, Wilaya ya Magharibi B, Mkoa wa Mjini Magharibi ikiwa pia ni kipindi ambacho Dunia inaadhimisha Wiki ya Maji.
Katika hotuba yake Rais Dkt. Mwinyi amesema kuwa, utekelezaji wa mradi huo uliowekwa jiwe la msingi ni katika kuyafikia malengo hayo huku akisisitiza kwamba hatua hiyo ni ndani ya miaka miwili tu na hana shaka ndani ya miaka mitano ijayo tatizo la maji litamalizika.
Amesema kuwa, takwimu zinaonesha kwamba hali ya upatikanaji wa maji nchini hivi sasa ni wastani wa asilimia 55 hadi kufikia mwaka huu wa 2022 na kueleza kwamba kukamilika kwa mradi huo asilimia zitaongezeka na kufikia 76 huku juhudi zaidi zikichukuliwa katika kuhakikisha wananchi wote wanapata maji safi na salama.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akimsikiliza Mkurugenzi Mkuu ZAWA, Dkt. Salha Mohamed Kassim akitoa maelezo ya Kitaalamu ya ujenzi wa Matenki ya Maji Safi na Salama Kwarara Kidutani, wakati wa hafla ya uwekaji wa Jiwe la Msingi la Mradi wa Uhuishaji na Uimarishaji wa Mfumo wa Usambazaji Maji Zanzibar, ikiwa ni Wiki ya Maji Duniani, kulia kwa Rais ni Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Mhe.Idrisa Mustafa Kitwana na kushoto kwa Rais Waziri wa Maji Nishati na Madini, Mhe. Shaib Kaduara.(Picha na Ikulu).
Rais Dkt. Mwinyi ametoa wito wa wizara husika pamoja na Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) kufanya kazi na kuwa wepesi wa kutatua changamoto za huduma hiyo zinazowakumba wananchi.
Amesisitiza kwamba, jukumu la ulinzi la miundombinu ya maji ni la watu wote na kueleza kwamba wananchi wana jukumu la kuilinda miundombinu hiyo na wasiwaruhusu watu wachache kuiharibu.
Aidha, Rais Dkt. Mwinyi amesema kuwa, upatikanaji wa huduma za maji safi na salama katika maeneo yote ya Unguja na Pemba ni miongoni mwa vipaumbele vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Hivyo, ameongeza kuwa jitihada zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali katika upatikanaji wa huduma za maji safi na salama ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya CCM ya mwaka 2020-2025, mipango mikuu ya maendeleo na ahadi zilizotolewa katika kipindi cha kampeni.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akiondoa kitambaa kuweka Jiwe la Msingi Mradi wa Uhuishaji na Uimarishaji wa Mfumo wa Usambazaji Maji Zanzibar, na kushoto kwa Rais ni Waziri wa Maji, Nishati na Madini Zanzibar, Mhe.Shaib Kaduara akiwa na viongozi wa Wizara na ZAWA wakishiriki kuondoa kitambaa,hafla hiyo imefanyika katika viwanja vya Mradi huo Kwarara Kidutani Wilaya ya Magharibi “B”Unguja, ikiwa sambamba na Maadhimisho ya Wiki ya Maji Duniani.(Picha na Ikulu).
"Leo tarehe 21, Machi 2022 tupo hapa Kwarara Mkoa wa Mjini Magharibi, kufungua ukurasa mwingine wa maendeleo ya sekta ya maji kwa kuweka jiwe la msingi la mradi mkubwa wa kuimarisha upatikanaji wa huduma za maji katika maeneo mbalimbali ambapo huduma hii haipatikani kabisa,"amesema Dkt.Mwinyi.
Rais Dkt.Mwinyi amesema kuwa, mradi huo utanufaisha zaidi maeneo ambayo kwa sasa yanaonekana kukua kwa haraka kutokana na wananchi wengi kujenga makazi yao mapya na kuhamia maeneo hayo ya Wilaya ya Magharibi A na Magharibi B pamoja na maeneo ya mpakani mwa Mkoa wa Mjini na Magharibi na Mkoa wa Kusini Unguja yakiwemo Tunguu, Jumbi na Ubago.
Amesema kuwa, maadhinisho hayo ambayo yanakwenda na ujumbe wa kauli mbiu isemayo Rasilimali za Maji chini ya Ardhi ni Nyenzo ya Kukabiliana na Mabadiliko ya tabianchi na kusisitiza kuwa na mipango mbadala na mikakati itakayowezesha kukabiliana na changamoto za aina tabianchi.
Wafanyakazi wa Kampuni ya L&T Construction wakimsikiliza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi (hayupo pichani) akihutubia katika hafla hiyo ya uwekaji wa Jiwe la Msingi la Mradi wa Uhuishaji na Uimarishaji wa Mfumo wa Usambazaji wa Maji Zanzibar, hafla hiyo imefanyika katika viwanja vya ujenzi matenki ya maji ya mradi huo Kwarara Kidutani Wilaya ya Magharibi “B”Unguja.(Picha na Ikulu).
Ameeleza kwamba hali ya tabianchi ndio inayopelekea uwezo wa uzalishaji wa maji katika vyanzo vilivyopo kupungua kama inavyoshuhudiwa katika vyanzo vya Mwanyanya na Mtopepo.
Amesisitiza kwamba katika hali kama hiyo ni lazima wananchi waendelee kupewa elimu ya kuvilinda na kuvitunza vyanzo vya maji kwa kuepuka ujenzi karibu na vyanzo hivyo na kuacha tabia ya ukataji wa miti na misitu pale vilipo.
Rais Dkt. Mwinyi ametoa wito kwa wananchi kuona haja ya kulipia maji ili huduma za maji ziwe endelevu na kuwataka ZAWA kuendelea kuweka mita za maji pamoja na kuhakikisha wanaotakiwa kulipa maji ni wale wanaoipata huduma hiyo na siyo kwa kila mwenye mfereji (bomba) ndani hata ikiwa maji hapati.
Wananchi wa Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja wakifuatilia hutuba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi (hayupo pichani) akihutubia wakati wa hafla ya uwekaji wa Jiwe la Msingi la Mradi wa Uhuishaji na Uimarishaji wa Mfumo wa Usambazaji wa Maji Zanzibar.(Picha na Ikulu).
Nae Waziri wa Maji, Nishati na Madini Shaib Hassan Kaduara ametoa pongezi kwa Rais Dkt. Mwinyi hukua akiahidi kwamba Wizara yake itaendelea kusimamia miradi yote ya maji ili kufikia lengo lililokusudiwa.
Nae Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Idrissa Kitwana Mustafa alieleza jinsi wananchi wa Mkoa huo pamoja na Mikoa jirani watakavyofaidika na mradi huo.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ZAWA, Meja Jenerali Issa Nassor alieleza jinsi mradi huo pamoja na miradi mengine ya maji itakavyotekelezwa na kuwataka wananchi kuwa walinzi wa miundombinu ya miradi yote ya maji.
Mapema Mkurugenzi Mkuu wa ZAWA, Dkt. Salha Mohammed alisema kuwa mradi huo unatekelezwa kwa ushirikiano wa pamoja kati ya Benki ya Exim pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akihutubia katika hafla ya Uwekaji wa Jiwe la Msingi la Mradi wa Uhuishaji na Uimarishaji wa Mfumo wa Usambazaji Maji Zanzibar, hafla hiyo imefanyika katika viwanja vya ujenzi wa matenki ya maji ya Mradi huo Kwarara Kidutani Wilaya ya Magharini “B” Unguja ikiwa sambamba na maadhimisho ya Wiki ya Maji Duniani.(Picha na Ikulu).
Amesema kuwa,mradi wote hadi kukamilika kwake utagharimu jumla ya Dola za Marekani Milioni 92.18 ambazo zimetolewa na Serikali ya India kupitia Benki ya Exim ya India kwa njia ya mkopo wa masharti nafuu kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Aliongeza kuwa hadi hivi sasa wastani wa shilingi 702,626,900 zimetolewa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ikiwa ni sehemu ya mchango wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa ajili ya gharama za malipo ya fidia kwa mali na mazao ya wananchi yaliyoathirika na ujenzi wa mradi huo pamoja na gharama za uendeshaji wa mradi.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akikabidhiwa zawadi maalum na Mwakilishi wa Kampuni ya L&T Construction, Bw.Hari Prakash, (kushoto kwa Rais) baada ya kumalizika kwa hafla ya Uwekaji wa Jiwe la Msingi la Mradi wa Uhuishaji na Uimarishaji wa Mfumo wa Usambazaji wa Maji Zanzibar, mradi huo wa ujenzi wa matangi ya maji katika eneo la Kwarara Kidutani Wilaya ya Magharibi “B” Unguja.(Picha na Ikulu).
Sambamba na hayo amesema kuwa, mradi huo umegawanyika sehemu tatu kwa utekelezaji wake ambapo sehemu ya kwanza itatekelezwa na Kampuni ya Megha Engineering Limited kutoka India na sehemu ya pili itatekelezwa na Kampuni ya Afcons and Vijeta-VJ ya India na sehemu ya tatu itatekelezwa na Kampuni ya Larsen& Toubro (L&T) Limited nayo ya India.
Nae Mwakilishi wa jimbo hilo Ali Ameir Mrembo kwa niaba ya wananchi wa jimbo hilo alitoa pongezi na shukurani kwa Rais Dkt. Mwinyi kwa kuwapelekea huduma hiyo muhimu katika kipindi kifupi alichokaa madarakani.