*Asisitiza faida za majadiliano,arejea hamasa ya kudumisha umoja, mshikamano, upendo na amani
NA MWANDISHI DIRAMAKINI
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amewasihi wanasiasa na wananchi kuangalia maneno wanayotoa midomoni mwao na athari zake kwa usalama wa nchi na mustakabali wa Wazanzibari.
Dkt.Mwinyi amesema, viongozi wana wajibu wa kuona umuhimu wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa iliyokuwepo nchini kwa maslahi ya taifa na wananchi wake.
Kauli hiyo ameitoa Machi 30,2022 wakati akizungumza na vyombo vya habari Ikulu jijini Zanzibar ikiwa ni utaratibu wake wa kila mwezi kuzungumza na vyombo hivyo.
Amesema, yapo maneno yanayotolewa kuhusu suala zima la uendeshaji wa nchi kuputia Chama cha ACT Wazalendo, mambo ambayo hayakupaswa kuzungumzwa hadharani na badala yake yalipaswa kuzungumzwa mezani kwa kukaa pamoja na kuwasilisha changamoto wanazoziona.
Rais Mwinyi amewasisitiza wanasiasa panapojitokeza tatizo basi ni vyema kukaa chini kujadili na kupata ufumbuzi ili waendeleze amani na mshikamano wao uliopo.
“Nimesimama hapa sina dhamira ya kujibu hata suala moja, lakini dhamira yangu ni kueleza kuwa ni vyema kama vyama vya siasa kuendeleza utaratibu wa kuzungumza changamoto kwa njia ya ambayo sio ya kushambuliana bali ni njia ya mazungumzo na majadiliano,”amesema Rais Dkt.Mwinyi.
Aidha, Rais Mwinyi amesema wana wajibu kama viongozi kuangalia maslahi mapana ya nchi, umoja na mshikamano wa wananchi huku akisisitiza umoja na mshikamano.
Amesema hakuna ambae hakumbuki wananchi wa Zanzibar walipotoka na walikuwa wana kila sababu ya kukaa meza moja ili kuzuia mambo ambayo yalikuwa yakitokea hususan katika kipindi cha uchaguzi sio mambo wazanzibar watapenda kuona yanaendelea.
“Sisi ni binadamu na hakuna aliyekamilika panapojitokeza tatizo ni wajibu wetu kama viongozi kukaa chini, kujadili na kuona tunapata ufumbuzi ya yale tunaona ni changamoto badala ya kukaa na kuzungumza maneno hadharani, mengine makali kabisa, shutuma na tuhuma ambazo hazijawekewa ushahidi jambo hilo naliona halifai,” amesema.Rais Mwinyi amesema yeye binafsi ameamua kutosimama kujibu wala kusimama kusema ya upande wa pili bali dhamira yake ni kuendelea kuwasihi wanasiasa na wanachi kudumisha amani, umoja na mshikamano wa nchi.
Amesema, yapo mambo ambayo yalikuwa yakijitokeza ikiwemo watu kupoteza maisha, kuwa wakimbizi, wanapeana talaka kwa sababu ya siasa kuchagua misikiti na mfarakano ulikuwa mkubwa hivyo wametoka huko na hawana nia ya kurudi.
Aidha, alibainisha dhamira na nia yake ya kuendeleza mshikamano kwa wananchi wa Zanzibar ipo pale pale na hana sababu ya kusimama na kujibu kwani haoni kwamba itawapeleka katika kuendeleza mshikamano na badala yake itazidi kuwafanya kufarakana jambo ambalo haoni kama litakuwa na mustakabali mzuri wa nchi.
Amesema, amani na mshikamano wa nchi ni muhimu kuliko jambo lolote kwani kuna mambo mengi yanazungumzwa ya kiuchumi na bila amani mambo hayo hayawezi kufanikiwa.
“Hakuna chochote kitakachoweza kutekelezeka bila ya kuwa na amani hivyo ni muhimu kuhakikisha kwamba amani yetu tunayo halafu mambo mengine yatakuja baadae,” amesisitiza.
Akizungumzia mabadiliko anayoyafanya katika Baraza la Mawaziri, Rais Dkt.Mwinyi amewahakikishia wananchi kuwa anafanya mabadiliko hayo chanya kwa lengo la kuleta ufanisi zaidi katika serikali.
Mbali na hayo, amesema serikali itahakikisha inafanya jitihada ili kuona bidhaa hazipandi bei hasa katika kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadhan hasa kwa zile zilizopunguziwa ushuru ikiwemo sukari.
Hata hivyo, Rais Dkt. Mwinyi alieleza hatua zilizofikiwa katika uchimbaji wa mafuta na gesi kupiga kampuni ya RAK GAS ambayo ilipaswa kuendelea na utafiti kwani tayari imeshafikia hatua ya 2D na sasa wamebakisha hatua mbili.
“Tunaendelea kuifuatilia kampuni hii ili kuhakikisha inakamilisha utafiti unaotakiwa kwa kufanya utafiti wa tatu na badaae kuchimba kisima ili kupata gesi,”amesema.
Sambamba na hayo, Rais Dkt.Mwinyi amesema amekuwa akitambua kuwa, timu ya watu wenye ulemavu Zanzibar imekuwa ikipata misada, lakini tatizo lipo kwa uongozi wao kwani upo wakati walisaidiwa, lakini hawakwenda safari.
Amesema, kitendo hicho kinaleta hofu na kutoaminiana ambalo sio jambo zuri na kubainisha kwamba hawawezi kuwahukumu watu wote kwa kosa la mtu mmoja bali ni vizuri kuweza kuona kwamba watu hao wanaendelea kusaidiwa na wakisaidiwa basi msaada unafika kwa walengwa na kufanya kilichokusudiwa.
Rais Mwinyi amesema jambo hilo ni kasoro, hivyo ni vizuri kuwekwa sawa ili kutowakosesha wengine wasiokuwa na hatia yoyote.