>Kutoka ukuu wa wilaya, Itikadi na Uenezi, ubunge hadi Ubalozi
NA GODFREY NNKO
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amemteua, Mheshimiwa Humphrey Hezron Polepole kuwa Balozi wa Tanzania nchini Malawi.
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Machi 14, 2022 na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais (Ikulu), Bi.Zuhura Yunus.
"Mheshimiwa Rais amewateua Bwana Humphrey Hezron Polepole kuwa Balozi wa Tanzania Nchi ya Jamhuri ya Malawi na Mhe. Shamsi Vuai Nahodha kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 Ibara ya 67(2) (g) ikisomwa pamoja na Ibara ya 71(1)(a),"imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Balozi mteule Polepole ataapishwa tarehe 15 Machi, 2022 saa 04:00 asubuhi viwanja vya Ikulu, Chamwino jijini Dodoma.
Aidha, kabla ya uteuzi huo, Mheshimiwa Polepole alikuwa Mbunge wa Kuteuliwa wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo uteuzi wake ulifanyika Novemba 29,2020 na aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dkt.John Pombe Joseph Magufuli.
Pia aliwahi kuhudumu nafasi mbalimbali ikiwemo ya Mkuu wa Wilaya ya Ubungo na baadaye aliteuliwa na Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kuwa Katibu wa Halmashauri Kuu Itikadi na Uenezi.
Ubalozi wa Tanzania nchini Malawi unaongozwa na Balozi Benedict Martin Mashiba ambaye aliapishwa Agosti Mosi, 2017 na aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dkt.John Pombe Joseph Magufuli ambapo alichukua nafasi ya Mhe.Victoria Richard Mwakasege ambaye alistaafu.