Rais Samia apeleka shangwe Kisiwa cha Jibondo,kwa mara ya kwanza wapata shule ya sekondari

NA MWANDISHI MAALUM,OR-TAMISEMI

UONGOZI wa Halmashauri ya Wilaya ya Mafia mkoani Pwani umetekeleza maagizo ya Katibu Mkuu Ofisi ya Rais- TAMISEMI, Prof. Riziki Shemdoe aliyoyatoa Desemba 27, 2021 ya kukamilisha ujenzi wa madarasa matatu ya awali ya shule ya sekondari katika Kisiwa cha Jibondo kwa ajili ya wanafunzi 53 waliofaulu kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2022.
Prof. Shemdoe wakati wa ziara yake wilayani Mafia tarehe 9 Machi, 2022 na kufika kisiwani Jibondo amemshukuru Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia na kutosha Shilingi Bilioni moja kwa ajili ya ujenzi wa sekondari itakayochukua wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi sita wa visiwa vya Jibondo, Chole na Juwani.

Akizungumza katika ziara yake, Katibu Mkuu huyo amesema alilazimika kuagiza kujengwa kwa madarasa matatu ya awali kwa ajili ya kuwapokea wanafunzi hao baada ya kuchaguliwa shule za Sekondari Kitomondo na Kilindoni ambazo ziliwalazimu kuvuka kwa maji ili kuzifikia shule hizo.
Kabla wanafunzi hao hawajaanza kusomea katika shule ya Jibondo walianza kusoma kwenye Shule ya Msingi Jibondo wakisubiria kukamilika kwa madarasa yao ili waweze kuhamia rasmi na kuanza masomo yao katika shule yao ya sekondari.

Prof. Shemdoe ameagiza uongozi wa Wilaya ya Mafia kuendelea kusimamia ujenzi wa majengo yaliyobakia ili ifikapo Julai, mwaka 2022 yakamilike kwa ubora unaotakiwa.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Mafia, Mhandisi Martin Ntemo amesema kazi hiyo ilifanyika kwa ushirikiano wa hali ya juu mpaka kukamilika kwake.

“Tulipoona changamoto ya upelekaji wa vifaa unaathiri zoezi la ujenzi tuliomba Kivuko cha Jeshi ambacho ndicho kilichotusaidia kupeleka vifaa vyote vya ujenzi na hata gari ya kwanza kufika Jibondo imepelekwa na kivuko hicho kwa ajili ya kuchukua vifaa kutoka feri mpaka eneo la ujenzi,” amesema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Wilaya ya Mafia, Kassim Ndumbo amesema, walipokea fedha za kujenga madarasa 10, nyumba za walimu ( 2 in 1 ) mbili, maabara tatu, jengo la utawala pamoja na vyoo vya walimu na wanafunzi.

Mkazi wa Jibondo, Aisha Mwindadi, amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwapelekea shule kwenye kisiwa hicho na imeokoa shilingi 2,000 walizokuwa wakitoa kila siku kwa ajili ya watoto wao kupanda boti kwenda na kurudi shule.
Ziara ya Prof. Shemdoe kisiwani Mafia ni ufuatiliaji wa maagizo aliyoyatoa Desemba 27,2021 kisiwani humo ambapo ni miongoni mwa maeneo magumu kufikika na huu umekuwa utaratibu wake kila mahali anapotoa maagizo kufuatilia utekelezaji wake.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news