NA MWANDISHI DIRAMAKINI
KIKOSI kazi cha kilichoteuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi kimependekeza mchakato wa kupata Katiba Mpya uanze baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, huku Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akikiagiza kulifanyia kazi na kupeleka mapendekezo.

Profesa Mukandara ametoa mapendekezo wakati akiwasilisha taarifa ya awali ya utendaji kazi wa kikosi hicho kwa Rais Samia Suluhu Hassan.
Kazi kubwa ya kikosi kazi hicho ni jukumu la kuangalia na kuchambua mwenendo wa hali ya demokrasia na namna ya kutatua changamoto zinazoikumba baadhi ya vyama vya siasa, ikiwemo mikutano ya hadhara.

Aidha, katika maelezo yake, Profesa Mukandara amesema, sababu za kutoa pendekezo hilo ni pamoja na kutoa fursa ya kuanisha dira mpya ya maendeleo ya miaka ijayo, itakayotoa mwelekeo wa katiba mpya.
“Pia kuna suala la kukosekana kwa muda wa kutosha kuanza kutumia Katiba mpya ndani ya kalenda ya uchaguzi 2025. Kuna haja ya kutoa fursa ya kufanya marekebisho ya sheria ya uchaguzi na kanuni zake. Jambo jingine ni kuna haja ya kutoa fursa ya kutosha ya kufanyia kazi masuala ya muda wa kati ikiwa ni pamoja na kuanisha masuala ya dira ya maendeleo,” amesema Profesa Mukandara.
Akizungumza baada ya kupokea taarifa hiyo, Rais Samia amesema kuwa, “Hili la Katiba mpya mtakwenda kulifanyia kazi na mtaleta mapendekezo yatakayotangazwa Watanzania wote wayaelewe.
"Mimi nakubaliana kuwa ni jambo la muda mrefu, lakini Watanzania wote waelewe. Lakini kwanza tukayafanyie kazi haya marekebisho tuliyoyasema haya kipindi hiki cha muda wa kati halafu huko mbele tuone je tuna haja ya kurekebisha katiba yetu pengine kutakuwa na haja sio ya kuandika mpya.
