NA MWANDISHI DIRAMAKINI
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema Serikali inafanya jitihada za kuweka mazingira rafiki ya kufundishia na kujifunzia ili kila Mtanzania anufaike na fursa za elimu kwa manufaa yake binafsi na taifa kwa ujumla.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Benjamin Mkapa, Emanuel Mzena mara baada ya kuwasili Shuleni hapo leo Machi 7, 2022 kwa ajili ya kuzungumza na Wanafunzi wa Shule hiyo. (Picha zote na Ikulu).
Rais Samia amesema hayo wakati alipotembelea Shule ya Sekondari ya Benjamin Mkapa na kuzungumza na wanafunzi wa shule hiyo, iliyopo Ilala jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na viongozi mbalimbali pamoja Wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Benjamin Mkapa, Wanafunzi wa Shule ya uhuru Mchanganyiko na Uhuru Msingi zilizopo eneo la Gerezani Ilala Jijini Dar es Salaam leo Machi 7, 2022.
Mhe. Rais Samia pia amesema Serikali imeendelea na Mkakati wa Kitaifa wa Elimu Jumuishi wa mwaka 2021/2022 hadi 2025/ 2026 ambao utazingatia utoaji elimu jumuishikatika ngazi zote za elimu ili kuwanufaisha pia wanafunzi wenye mahitaji maalumu.
Pamoja na kujenga shule na madarasa ya wanafunzi wenye mahitaji maalum na jumuishi, Serikali imeshatumia zaidi ya shilingi bilioni 5.9 kununua vifaa kwa ajili ya wanafunzi hao katika elimu ya msingi, sekondari na vyuo.
Mbali na hapo, Serikali imetoa mafunzo ya aina tofauti kwa walimu 3980 wenye taalumaya Elimu Maalum katika ngazi ya Msingi, Sekondari na Ualimu.
Mafunzo hayo yametolewa kwa wadhibiti ubora ili waweze kukagua madarasa maalum na jumuishi pamoja na miundombinu kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalum.