NA GODFREY NNKO
WAZIRI wa Fedha na Mipango,Mheshimiwa Dkt.Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) amesema kuwa, miongoni mwa mfanikio ya ziara za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan katika nchi za Ubelgiji, Ufaransa na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) ni pamoja na kiuchumi, diplomasia na kijamii.
Pia amesema, ziara hizo zimeonesha matokeo makubwa si tu kwa Serikali bali pia katika sekta binafsi nchini na kupitia ziara hizo kila nchi na kila taasisi ilikuwa inatafuta fursa ya kukutana na Rais Samia ili kuona namna ya kuja kuwekeza nchini.
Mheshimiwa Dkt.Nchemba ameyasema hayo leo Machi 2, 2022 wakati akizungumza katika mjadala wa Kitaifa ulioratibiwa na Watch Tanzania kupitia Mtandao wa Zoom kwa udhamini wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) na Airtel Tanzania.
Kupitia mjadala huo ambao umewakutanisha pamoja viongozi na wadau mbalimbali wa maendeleo ulikuwa unaangazia Mafanikio ya ziara zilizofanywa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan katika nchi ya Ufaransa, Ubelgiji pamoja na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) huko Dubai.
"Mheshimiwa Rais amefunguwa kwa kiwango kikubwa sana diplomasia ya kiuchumi katika ujenzi wa uchumi wa kisasa katika karne ya leo. Kwa hiyo Mheshimiwa Rais ameiwezesha nchi kupanua diplomasia ya kiuchumi ambayo ni uelekeo mpya wa kisera kwa nchi hususani katika mambo ya nje kwa mataifa mengi duniani. Katika kuendeleza ushirikiano wetu na mataifa mengine,"amnesema Mheshimiwa Dkt.Nchemba.
Amesema kuwa,kupitia ziara hiyo nchi, taasisi ambazo zinashughulika na masuala ya mikopo, misaada na uwekezaji yakiwemo makampuni na jumuiya za wafanyabiashara wameonesha utayari wa kushirikiana na Tanzania katika nyanja mbalimbali.
Mheshimiwa Waziri Dkt.Nchemba amesema kuwa, mwitikio huo unaonesha kuwa, baada tu ya ziara hiyo ya Mheshimiwa Rais Samia, Tanzania inatarajia kupokea ugeni mkubwa ambapo hali hiyo itawezesha kupata misaada na mikopo nafuu ikiwemo kuongezeka uwekezaji hatua ambayo itafungua fursa za ajira na kustawisha uchumi wa nchi.
"Kwa hiyo,ziara hizi za Mheshimiwa Rais zina mafanikio ya kiuchumi, diplomasia na kijamii na pia ziara hii imegusa pia sekta binafsi na sio Serikali peke yake. Kutokana na ziara hizi matarajio yetu ni kuongezeka kwa mikopo nafuu, misaada pamoja na kuongezeka wigo wa kodi kupitia uwekezaji ambao ni injini kubwa ya uchumi nchini, hivyo itaongeza idadi kubwa ya ajira nchini,"amsema Waziri.
Amesema, awali Mheshimiwa Rais alikutana na viongozi waandamizi wa taasisi za Kimataifa ikiwa ni hatua moja wapo ya kuimarisha ushirikiano wa Kimataifa ambao una tija kubwa kiuchumi, kijamii na maendeleo.
Amesema, kwa upande wa Ulaya jumla ya mikataba sita ya miradi ya mikopo nafuu pamoja na misaada yenye thamani ya shilingi trilioni 1.77 kwa upande wa Serikali ilisainiwa.
Amesema, mikaba hiyo inahusisha Mkataba wa Awali kati ya Serikali ya Jamhuri ya Ufaransa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ajili ya kugharamia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimkakati nchini.
Pia mkataba wa mkopo wa masharti nafuu kati ya Serikali ya Jamhuri ya Ufaransa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ajili ya kugharamia mradi wa ujenzi wa barabara ya mabasi yaendayo haraka.
Mheshimiwa Waziri amesema, mkataba mwingine ni mkopo wa masharti nafuu kati ya Serikali ya Jamhuri ya Ufaransa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ajili ya kuimarisha Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania ili kufikia malengo ya kutoa mikopo ya muda mfupi na mrefu kwa sekta ya kilimo
Miradi mingine kulingana na fedha hizo ni kwa ajili kuimarisha mifumo ya kidijitali,ustawi wa jamii ya Watanzania kwa kuzingatia usawa wa jinsia na kuimarisha miji.
Mheshimiwa, Waziri Dkt.Nchemba amesema kuwa, mafanikio mengine ya ziara hizo katika Umoja wa Falme za Kiarabu (UEA) huko Dubai ni pamoja na kushuhudia katika mkutano wa kibiashara hati 12 zikisainiwa kati ya Serikali ya Tanzania kupitia wizara na taasisi mbalimbali za uwekezaji mbalimbali sekta binafsi.
"Aidha, hati zingine 23 zimetiwa saini kati ya makapuni kutoka Tanzania na makampuni mengine ambayo yatashirikiana na sekta binafsi kwa ajili ya kukuza uchumi nchini kwetu na mafanikio mengine katika ziara hii ni kupatika kwa ajira zaidi ya laki mbili katika kipindi cha miaka minne.
"Uwekezaji huo utatarajiwa kugharimu zaidi ya dola za Kimarekani bilioni 7.47 ambazo ni sawa na shilingi trilioni 17.35 za Kitanzania,"amesema.
TIC
Akizungumza katika mjadala huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Dkt.Maduhu Kazi amesema kuwa, wao walikuwa katika ziara hiyo wakiwa na mambo mawili.
"Sisi tumekuja kwenye ziara hizo tukiwa na mambo mawili mapana, kwamba tuchangie kwenye Diplomasia ya Uchumi kwa kuweza kushirikiana na Mheshimiwa Rais (Samia Suluhu Hassan) pamoja na mawaziri kufanya kitu kinaitwa balance sustainable investment approach (kustawisha mbinu za uwekezaji endelevu) ya kwamba tuweze kushiriki kutangaza na kupata uwekezaji mpana zaidi katika sekta mbalimbali.
"Vile vile tuweze kupata uwekezaji katika nchi nyingine ambazo kwa kihistoria hazipo sana kwenye picha ya uwekezaji kwa nchi ya Tanzania, hayo yote mawili tumeyachukua na kuongeza lingine kwamba, ushiriki wa Tanzania unakuwa wa kutosha,"amesema.
Amesema, kupitia ziara hizo kumekuwa na mafanikio mbalimbali kuanzia sekta ya kilimo ambapo kuna miradi mbalimbali, nishati, ujenzi, uchukuzi, mafuta, gesi na nyinginezo.
Pia amesema kuwa, wamekuwa na wakati mzuri wa kushirikisha miradi zaidi ya 100 kupitia njia ya teknolojia ya kisasa kwa kutumia QRCode ambayo iliwezesha wawekezaji kupata taarifa kwa urahisi.
Dkt.Kazi amesema kuwa, kupitia maonesho ya DubaiExpo nchi ya Tanzania imetambulika ipo mbele kwa upande wa teknolojia jambo ambalo ni muhimu zaidi katika sekta ya uwekezaji.
"Hilo lazima niliseme kwa sababu kulikuwa na kampuni walitaka (zilitaka) kutusaidia katika masuala ya utoaji huduma na tulivyowaambia kuwa tayari tunayo hawakuamini na tulichofanya tukawaambia wafunge safari waje wajionee wenyewe.
"Na TIC tulikuwa tumeshiriki kwenye maonesho haya ya EXPO Dubai tangu yalipoanza Oktoba 1 na hapo ndipo tulianza kwa kuwaandaa wawekezaji na walihamasika sana na tumeshaanza kupokea wawekezaji ambao wana nia ya kuja kuwekeza kuanzia wiki hii na ijayo,"amesema Dkt.Kazi.
Pia amesema kuwa, kusainiwa kwa mikataba iliyogusa sekta mbalimbali ikiwa na thamani ya zaidi ya shilingi trilioni 17.35 ni kielelezo kikubwa kuwa uwekezaji wa Tanzania umekubalika.
"Na watu wamekubali kutokana na mazingira ambayo yamekuwa ni chanya kuruhusu uwekezaji na sisi TIC tumejiandaa kupokea hao wawekezaji.
"Tulikuwa na matarajio kwamba, tutakuwa na wawekezaji 200, lakini kikao cha kwanza walikuwa 400. Tukaweka makadiro kwamba ni 409, lakini wakawa zaidi ya 600, kwa hiyo utaona kwamba kwa kweli Mheshimiwa Rais wito wake wa uwekezaji na kuifungua Tanzania upya umepokelewa kwa namna ya ajabu sana na sisi wote imetushangaza,"amesema Dkt. Kazi.
Waziri wa Nishati
Kwa upande wake Waziri wa Nishati, Mheshimiwa January Makamba amesema kuwa, ziara za Rais Samia nje ya nchi zina umuhimu mkubwa katika nyanja mbalimbali ikiwemo kiuchumi.
Amesema kuwa, kila mmoja anashuhudia namna ambavyo mapokezi ya Rais Samia huko nje yalivyo makubwa ikiwa ni ishara kwamba nchi ya Tanzania bado inaaminika zaidi duniani.
"Mheshimiwa Rais mapokezi anayopata kule anakoenda na mikutano anayofanya inaonesha kwamba nchi yetu bado inaaminika na kuthaminiwa na pia kiongozi wetu anaaminika na zaidi ya yote, haya yanatengeneza fursa nchini kwetu,"amesema.
Amesema, kwa upande wa wizara yake kupitia ziara za Mheshimiwa Rais wamefanikiwa kusaini mikataba kadhaa ukiwemo wa Kampuni ya Master.
"Kampuni ya Master ni moja ya makampuni matatu duniani ya nishati jadidifu, tumekubaliana kuingia makubaliano na TANESCO kuunda kampuni ya pamoja kwa ajili ya uzalishaji umeme wa kutumia jua, upepo na joto ridi,"amesema.
Mkataba mwingine, Mheshimiwa Makamba amesema ni kati ya Kampuni ya Abu Dhabi National Bord ambayo imeingia mkataba baina ya Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC) ili kupata mafuta kwa bei nafuu.
Sambamba na mkataba na Kampuni ya DP World ambapo wamekubaliana kuhusu uwekezaji kwenye hifadhi ya mafuta.
"Yaani matenki na miundombinu ya upakuaji na uhifadhi wa matufa pale bandarini,"amesema Mheshimiwa Waziri huku akisisitiza kuwa, nchi yetu bado ina mahitaji ya mitaji, teknolojia na maarifa ili kusukuma maendeleo yake mbele.
"Hivyo, katika hizi ziara za Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan imetusaidia kupata mitaji, uwezekano wa kubadilishana teknolojia na maarifa, hivyo kuzalisha ajira, kukua uchumi na hatimaye kuleta maendeleo kwa Watanzania. KWA WACHANGIAJI ZAIDI TAZAMA HAPA CHINI;
M