NA MWANDISHI DIRAMAKINI
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema Serikali itaendelea kuendeleza mazuri yote yaliyoachwa na Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli pamoja na kuleta mema mengine mapya.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiweka Shada la Maua katika Kaburi la Aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli mara baada ya Misa Takatifu iliyofanyika katika uwanja wa Michezo wa Magufuli tarehe 17 Machi, 2022. (Picha na Ikulu).
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akimfariji Mama Janeth Magufuli baada ya kuweka Shada la Maua katika Kaburi la Aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano Hayati Dkt. John Pombe Magufuli mara baada ya Misa Takatifu iliyofanyika katika uwanja wa Michezo wa Magufuli tarehe 17 Machi, 2022.
Rais Samia amesema hayo Machi 17,2022 wakati wa maadhimisho ya kumbukizi ya mwaka mmoja ya kifo cha aliyekuwa Rais Hayati, Dkt. John Magufuli Wilayani Chato Mkoani Geita.
Mhe. Rais Samia amemwelezea Hayati Magufuli kuwa Kiongozi aliyepinga rushwa na ubadhirifu, na kusisitiza uchapakazi na uzalendo kwa Taifa.
Rais Samia amewaahidi wananchi wa Chato kuwa Serikali itakamilisha na kushiriki kuifungua miradi yote ya maendeleo ambayo imeshakamilika ikiwemo stendi mpya ya Chato, uwanja wa ndege wa Chato uliofikia asilimia 95 pamoja na kivuko cha Chato.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akisaini kitabu cha kumbukumbu kabla ya kuweka Shada la Maua katika Kaburi la Aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano Hayati Dkt. John Pombe Magufuli katika Kumbukizi ya Mwaka mmoja tangu kufariki dunia kwa Hayati Dkt. Magufuli tarehe 17 Machi, 2022.
Vile vile, Rais Samia ametoa wito kwa wananchi wote kuendelea kuelimishana na kuhamasishana kushiriki katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi litakayofanyika Agosti, 2022.