RC Hapi aagiza watu 100 mkoani Mara wanaodaiwa kuhusika na wizi wa fedha mbichi za Serikali wakamatwe

NA FRESHA KINASA

MKUU wa Mkoa wa Mara, Mheshimiwa Ally Hapi ameliagiza Jeshi la Polisi mkoani humo kuwakamata watu zaidi ya 100 katika halmashauri za mkoa huo wanaodaiwa kuhusika na wizi wa fedha mbichi za Serikali huku orodha nyingine ya watu ambao wamehusika na wizi huo akiomba akabidhiwe majina yao kwa hatua za kisheria.
Ameyasema hayo leo Machi 3, 2022 katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya mkoa huo kilichofanyika Ukumbi wa Uwekezaji wa Mkoa wa Mara, ambapo pamoja na mambo mengine amesema kuwa hayuko tayari kuona fedha za Serikali zikiliwa na watu wachache na kushindwa kuwanufaisha wananchi.

Amesema kuwa, watu hao wamekusanya fedha za Serikali na mfumo umeonesha idadi ya fedha walizokusanya, lakini jambo la kishangaza ni kwamba, hawajaweka benki fedha zote, wengine wameweka kiasi, nyingine hawajaweka, jambo ambalo linafifisha juhudi za Serikali za kuwaletea maendeleo wananchi.

"Nilitoa maelekezo wiki mbili watu ambao walikuwa hawajaweka fedha benki baadhi yao kule Sirari tuliwabana mtu mmoja amelipa milioni tano, baada ya ndugu zake kuchangia. Sina mchezo katika kusimamia fedha za umma, niliwaomba Wakurugenzi katika baadhi ya halmashauri wabadilishe watu wa kukusanya, lakini halmashauri zingine bado hazijafanya hivyo. Naomba majina yote ya watu waliohusika ambao wameweka nusu fedha kusudi wachukuliwe hatua za kisheria, lengo ni kunusuru fedha za serikali zilete tija kwa wananchi tutakamata hata watu 200,"amesema Hapi.

Amezitaka pia Halmashauri za Mkoa huo kuongeza kasi ya ukusanyaji wa mapato na upelekaji wa fedha za maendeleo kutekeleza miradi mbalimbali katika maeneo yao kwa maslahi mapana ya wananchi. Na akasisitiza pia watendaji wa serikali wanapaswa kufanya kazi kwa weledi na kujikita kushughulikia kero za wananchi katika maeneo yao.
 
Katika hatua nyingine Hapi amewataka viongzozi wote mkoani humo kuanzia ngazi za chini kuwashirikisha kikamilifu wananchi washiriki katika zoezi la uwekaji wa anuani za makazi kwa ufanisi akisisitiza kuwa, zoezi hilo linapaswa kukamililika ifikapo mwezi Aprili, mwaka huu.

"Anuani za makazi ni muhimu sana, operesheni hii ilitangazwa na Mheshimiwa Rais mwezi Februari mwaka huu. Nimeendelea kufuatilia na nimeona hatua za ushirikiswaji wananchi, watendaji kwa ngazi za chini likiendelea vizuri, Mkoa wa Mara mwezi wa nne tuwe tumemaliza, viongozi wote tuwashirikishe wananchi,"amesema Mheshimiwa Hapi.

"Nashangaa halmashauri za mji na manispaa kuona bado mnasuasua wakati mitaa imepengwa, maeneo ya jografia yamepangwa vyema, sioni kwa nini mpaka sasa bado hazijakamilisha ili tuzindue. 
 
"Manispaa ya Musoma, Tarime Mji, Bunda Mji, jambo hili tulibebe kwa uzito wake Rais amepunguza gharama kutoka shilingi Bilioni 728 ambazo zingetumika hadi Biolioni 28 ili fedha zingine zifanye maendeleo kwa wananchi. Zoezi hili litajumuisha mitaa, ata, barabara na namba za nyumba na katika Sensa ya Watu na Makazi litasaidia sana,"amesema Mheshimiwa Hapi.

Pia, Hapi amesema zoezi la Sensa ya Watu na Makazi litakuja kutumia taarifa zilizokusanywa kwenye anuani za makazi na hivyo amewataka pia viongozi katika maeneo yao kuwahamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi pindi muda wake ukiwadia.

Katika kikao hicho cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Mara (RCC) Mkoa umependeleza kwa mwaka wa fedha 2022/2023 umeomba kuidhinishiwa kukusanya na kutumia Jumla ya shilingi Bilioni 312.23 Kati ya fedha hizo shilingi Bilioni 217.61 ni matumizi ya kawaida na Shilingi Bilioni 94.62 ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo itokanayo na makusanyo ya vyanzo vya ndani.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news