RC Hapi aanika mafanikio yaliyopatikana mkoani Mara, mwaka mmoja wa Rais Samia madarakani

*Bilioni 13/- zapokelewa kwa ajili ya Mpango wa Elimu Msingi bila Malipo

NA FRESHA KINASA

MKUU wa Mkoa wa Mara, Mheshimiwa Ally Hapi amebainisha mafanikio katika sekta mbalimbali yaliyopatikana mkoani humo kwa kipindi cha mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ambaye alichukua nafasi ya mtangulizi wake hayati Dkt.John Pombe Joseph Magufuli.
Mheshimiwa Hapi ameeleza mafanikio hayo leo Machi 25, 2022 katika ukumbi uliopo katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma,ambapo pamoja na mambo mengine amesema wananchi wa Mkoa wa Mara wamenufaika na maendeleo yalitotekelezeka kwa mwaka mmoja tangu Rais Samia aingie madarakani.

Amesema, mafanikio hayo yamegusa nyanja za kiuchumi,kijamii na kuufanya mkoa huo uzidi kupiga hatua mbele za kimaendeleo.

Mheshimiwa Hapi amesema, katika kipindi hiki watumishi 8,148 wa Mkoa wa Mara wamepandishwa vyeo, huku watumishi 257 wamebadilishiwa kada jambo ambalo limeongeza ari kwa watumishi na kuwafanya kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi mkubwa katika kuwatumikia wananchi.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2021/2022, hadi kufikia Februari 2022, Halmashauri za Mkoa wa Mara zimetoa mikopo kwa vikundi 187 yenye thamani ya shilingi 1,117,587,995 sawa na asilimia 97 ya fedha iliyopaswa kutolewa kutokana na makusanyo ya ndani.

“Vikundi viivyonufaika na mikopo hii ni vikundi 92 vya wanawake, vikundi 53 vya vijana na vikundi vya watu wenye ulemavu 42,”amesema Mheshimiwa Hapi.

Aidha, Mheshimiwa Hapi ameeleza kuwa Mkoa wa Mara umetengewa jumla ya shilingi bilioni 22. 469 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya sekta ya elimu (shilingi bilioni 14.32), afya (shilingi bilioni 6.88) na maji (shilingi bilioni 5.78).

“Katika miradi ya afya, shilingi bilioni 4.803 ni kwa ajili ya Hospitali ya Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere iliyopo Kwangwa Mjini Musoma, shilingi bilioni 2.08 ni kwa ajili ya kutekeleza miradi ya ujenzi na ukarabati wa vituo vya kutolea huduma za afya katika Mamlaka za Serikali za Mitaa,”amesema Mheshimiwa Hapi.

Mheshimiwa Hapi ameeleza kuwa Mkoa wa Mara pia umetengewa shilingi billioni 8.362 fedha za ruzuku kutoka serikalini kwa ajili ya kutekeleza miradi ya ukamilishaji wa ujenzi wa Hospitali za Hamashauri za Wilaya ya Bunda, Butiama, Musoma, Rorya, Tarime (Nyamwaga) na Serengeti. Na pia ujenzi wa vituo vya afya 15 na ukamilishaji wa zahanati 26 na nyumba 3 za watumishi.

"Aidha, katika kipindi hiki Mkoa wa Mara umepokea shilingi bilioni 3.750 zinazotokana na miamala ya simu kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya 10 kwa ajili ya kujenga majengo ya wagonjwa wa nje (OPD), maabara, kichomea taka, jengo la kufulia, mionzi, nyumba ya watumishi (3 in 1), na njia za kupita,"amesema Mhe.Hapi.

Mheshimiwa Hapi ameeleza kuwa hali ya upatikanaji wa dawa muhimu kimkoa umeongezeka na kufikia asilimia 92.3 hadi mwezi Machi, 2022 na hii imetokana na halmashauri kutumia vyanzo mbalimbali vya fedha kwa ajili ya manunuzi ya dawa, vifaa tiba na vitendanishi.

Kwa upande wa elimu, mkoa umepokea shilingi bilioni 4.7 kwa ajili ya ujenzi wa Shule za Sekondari za kata mpya 10 kupitia Programu ya Kuboresha Elimu ya Sekondari (SEQUIP) na ujenzi wa miradi unaendelea. 

Huku akisema, Mkoa wa Mara umepokea jumla ya shilingi bilioni 13 kwa ajili ya Mpango wa Elimu Msingi bila Malipo tangu Serikali ya Awamu ya Sita ilipoingia madarakani.

Amesema, mkoa umepokea jumla ya shilingi bilioni 8.107 fedha za miradi ya maendeleo ya elimu kutoka Serikali Kuu, EP4R, SRWSS, na GPE-Lanes kwa ajili ya miradi mbalimbali ya elimu.

Mheshimiwa Hapi ameeleza kuwa, katika Sekta ya Maji, upatikanaji wa huduma za maji safi ni za uhakika na kwa sasa miradi kadhaa inaendelea kutekelezwa ili kuboresha huduma za upatikanaji wa maji kwa maeneo ya mijini na vijijini.

Miradi hiyo ni mradi wa ujenzi wa tanki la Bhalima na miundombinu ya kusafirisha maji shilingi bilioni 8.5, mradi wa ujenzi wa chujio la maji katika Mji wa Mugumu shilingi bilioni 3.121, mradi wa ujenzi wa chujio la maji Bunda Mjini shilingi bilioni 10.6, mradi wa usambazaji wa maji katika vijiji vya Mbalibali na Kitunguruma katika Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti shilingi milioni 748.50.

Pia, mradi wa ukarabati wa miundombinu ya maji katika Mji wa Shirati Wilaya ya Rorya shilingi milioni 409 mradi wa maji wa Mugango- Kiabakari- Butiama shilingi bilioni 70.863 ambao Mheshimiwa Rais Samia alipofanya ziara mkoani Mara aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa Mradi huo mkubwa na wa kihistoria.

Mheshimiwa Hapi ameeleza kuwa ili kuboresha huduma za maji vijijini Mamlaka ya Maji Vijijini (RUWASA) Mkoa wa Mara imekamilisha miradi ya maji 51 yenye thamani ya shilingi bilioni 15, ambayo inahudumia vijiji 193 na kuongeza upatikanaji wa maji kutoka asilimia 59.1 hadi asilimia 65.6.

“Kwa mwaka huu wa fedha RUWASA imetengewa shilingi bilioni 19.757 kwa ajili ya kutekeleza miradi 65 ambapo miradi 29 ni miradi mipya, 12 ni miradi ya upanuzi, 17 ni miradi ya ukarabati wakati 7 ni miradi ya utafutaji wa vyanzo vya maji,”amesema Mheshimiwa Hapi.

Mheshimiwa Hapi ameeleza kuwa kwa kwa upande wa sekta ya Nishani, upatikanaji wa umeme katika maeneo ya Mjini ni wa uhakika na kupitia mradi wa REA, jumla ya vijiji 407 vimepata umeme na vijiji 45 vipo katika Mpango wa REA awamu ya tatu mzunguko wa pili ambao utagharimu shilingi bilioni 9.4.

Katika Sekta ya Madini, katika kipindi cha Julai 2021 hadi Februari, 2022 Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa imekusanya dhahabu kilo 9,970.68 yenye thamani ya shilingi 1,017,594,887,992.08, madini ya ujenzi yenye tani 16,426.86 yenye thamani ya shilingi bilioni 2.070; na makenikia ya dhahabu kilo 475,130 yenye thamani ya shilingi bilioni 5.948.

“Aidha katika kipindi hiki, jumla ya kilomita za mraba 103.871 zimetengwa kwa ajili ya wachimbaji wadogo katika Mamlaka za Serikali za Mitaa na jumla ya lesseni 213 za uchimbaji mdogo wa madini zimetolewa,”amesema Mhe.Hapi.

Kwa upande wa barabara zinazosimamiwa na Mamlaka ya Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA), jumla ya shilingi bilioni 25.667 zimetengwa kwa ajili ya matengenezo ya barabara na vivuko katika serikali za mitaa. 

Ambapo kufikia Machi, 2022 jumla ya mikataba 87, ya ujenzi na ukarabati wa barabara yenye thamani ya shilingi bilioni 21.961 imesainiwa na ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji.

Kuhusiana na barabara zinazosimamiwa na Wakala wa Barabara (TANROADS) Mheshimiwa Hapi amesema kuwa, Mh.Rais Samia ameongeza bajeti ya barabara kutoka shilingi bilioni 21.82 hadi kufikia shilingi bilioni 22.08.

“Aidha Serikali imetenga fedha za ujenzi wa uwanja wa ndege Musoma utakaogharimu shilingi bilioni 35.048 na malipo ya fidia kupisha upanuzi wa uwanja kwa wakazi 86 kiasi cha shilingi bilioni 4.337,”amesema Mhe.Hapi.

DIRAMAKINI BLOGDira imefanya mazungumzo na baadhi ya wananchi wa Musoma akiwemo Paul Yusuph mkazi wa Kata ya Bweri amesema anapongeza juhudi za maendeleo zinazofanywa na Mheshimiwa Samia Hassan katika Mkoa wa Mara ikiwemo utoaji wa fedha nyingi za kugharamia miradi ya maendeleo hasa upande wa maji vijijini.

"Niombe Mheshimiwa Ally Hapi ambaye amepewa jukumu la kusimamia maendeleo ya Mkoa wa Mara asirudi nyuma, aendelee na moto ule ule wa kushughulikia watendaji na Watumishi ambao wanafanya mchezo na fedha za serikali. Tunahitaji kuuona Mkoa wa Mara ukizidi kupaa kimaendeleo fedha zisimamiwe kikamilifu kuleta zilete matokeo chanya,"amesema Mathias Juma.

Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan aliapishwa Machi 19,2021 kuwa Rais wa Awamu ya Sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya kifo cha aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kilichotokea Machi 17, 2021.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news