NA FRESHA KINASA
MKUU wa Mkoa wa Mara,Ally Hapi amesema kuwa, kwa sasa hana mchezo na watendaji ama watumishi ambao wanakwamisha juhudi za Serikali za kuwaletea maendeleo wananchi.
Hapi amesema kuwa, hataogopa kumchukulia hatua kiongozi mzembe, fisadi, ama mla rushwa ambaye atabainika kufanya mambo ya ovyo na yasiyo na tija kwa maendeleo ya wananchi.
Ameyasema
hayo leo Machi 2, 2022 wakati akizungumza katika kikao cha Bodi ya
Barabara kilichofanyika katika Ukumbi wa Uwekezaji Mjini Musoma mkoani
Mara, ambapo pamoja na mambo mengine amesema Serikali imekuwa ikifanya
jitihada kubwa za kuwaletea maendeleo wananchi ikiwemo kutoa fedha za
miradi ya maendeleo lazima ziwanufaishe wananchi.
"Kama
kuna mtumishi anakula na mtu fulani nitamshughulikia kikamilifu na
hakuna simu itakayopigwa. Rais anataka mkoa ubadilike, upige hatua
kimaendeleo, mambo ya wizi au rushwa yaachwe. Mimi mwenzenu saizi nina
raha kweli kweli nimekabidhiwa rungu na Mheshimiwa Rais sitaogopa
kumchukulia hatua kiongozi yeyote bila kumuonea. Lazima tuweke msingi
mzuri katika kuwatumikia wananchi wetu,"amesema Mheshimiwa Hapi.
"Kama viongozi wenzangu ndani ya Mkoa wa Mara hatutabadilisha mkoa huu kwa sasa hatutaweza kubadilisha wakati mwingine. Kama kuna tatizo tunalitatua na tunasonga mbele kwa pamoja, itafika wakati tuanze kushughulika na watu wanaochafua mkoa wetu, vijana acheni kutumika. Vyombo vya dola ingizeni makachero kwenye makundi hayo yanayofarakanisha watu bila ukweli wowote kusudi wanaofanya hivyo wachukuliwe hatua kali. Lazima tujenge msingi wa uadilifu haiwezekani kijana kuchafua mkoa kwa masilahi yake badala ya kufanya kazi za maendeleo,"amesema Hapi.