NA ROTARY HAULE
MKUU wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge amewaangukia wananchi wa Kijiji cha Visezi Kata ya Vigwaza katika Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze kuruhusu mradi wa ujenzi wa barabara ya Vigwaza-Kwala kuendelea wakati Serikali ikiwa inashughulikia malalamiko yao ya kulipwa fidia.
Barabara hiyo inajengwa kwa kiwango cha zege kwa barabara mbili kwenda na barabara mbili kurudi.
Wananchi wa Visezi wamekuwa wakilalamika juu ya kulipwa fidia kwa ajili ya kupisha mradi huo hali ambayo imepelekea mradi huo kusimama na hivyo mkandarasi kuwa katika wakati mgumu wa kutekeleza majukumu yake.
Akizungumza katika mkutano wake na wananchi wa eneo hilo uliofanyika leo Mkuu huyo wa mkoa amesema kuwa, ziara yake kijijini hapo imelenga kuleta ustawi wa wananchi na Serikali yao hasa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Kunenge amesema kuwa, mradi wa ujenzi wa barabara ya Vigwaza - Kwala unatumia fedha nyingi kiasi cha shilingi Bilioni 31 na endapo ukikamilika utakuwa manufaa makubwa kwa wananchi wa eneo hilo na Taifa kiujumla.
Amesema,barabara hiyo ni ya kimkakati na ina umuhimu mkubwa kwa kuwa inaelekea katika Bandari ya Nchi Kavu (Dry Port) inayojengwa Kwala pamoja na mradi mwingine wa uwekezaji (Industrial Park) ambayo utakuwa mkubwa Afrika.
Kunenge amesema kukamilika kwa barabara hiyo pamoja na miradi hiyo itakuwa na manufaa makubwa kwa wananchi hususani wa Vigwaza na Kwala kupata ajira pamoja na kuongeza mapato ya Taifa kupitia kodi zitakazokuwa zinakusanywa kupitia miradi hiyo.
Amesema,hakuna sababu ya wananchi kuzuia ujenzi wa barabara hiyo kwasababu hawajalipwa fidia kwani kufanya hivyo ni aibu kubwa kwa Taifa na kwamba waache mradi huo uendelee huku changamoto yao ikifanyiwa kazi.
Aidha, Kunenge ameongeza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan anafanyakazi kubwa kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wake na wananchi wa Vigwaza-Visezi- Kwala wamepata bahati kubwa ya mradi huo hivyo kinachotakiwa ni kuhakikisha wanaruhusu mradi kutekelezwa kwa faida yao.
"Nimekuja hapa kuwaambia mambo makubwa mawili,kwanza kuwaeleza umuhimu wa mradi huu na pili kuwaomba muwe watulivu kwa kuwa Serikali inashughulika na jambo lenu na sio busara kuzuia mradi wa Bilioni 31 kwa sababu ya fidia,"amesema Kunenge.
Kunenge amesema kuwa, Bandari Kavu inajengwa kwa gharama ya Sh.Bilioni 37 huku ekari 4000 zitatumika kujenga mradi mkubwa wa viwanda Afrika ambapo mpaka sasa tayari mkandarasi amepatikana na amepewa ekari 2500.
"Serikali inategemea mradi huu kutoa ajira,kodi na kuendelea kutoa huduma za jamii kwa wananchi ikiwemo maji,afya ,umeme na huduma nyingine lakini barabara imesimama kwa ajili ya wananchi kulipwa fidia,hii si sawa,lakini eneo hili linaenda kuwa Mji mkubwa ambao utasaidia watoto kuwa na maisha mazuri,"ameongeza Kunenge.
Kunenge amesema, Serikali inalifanyia kazi suala la fidia wanayolalamikia na muda si mrefu watapata majibu sahihi ya Serikali endapo wanastahili fidia au hawastahili lakini kikubwa ni kuhakikisha mradi wa ujenzi wa barabara hiyo unaendelea.
"Nimekuja hapa Mkuu wa Mkoa wa Pwani, mwakilishi wa Rais na sisi tunafanya kazi ya kuwasaidia wananchi na nyinyi ninaamini niwaelewa,naomba mnipe imani mimi mkuu wenu kwa kuwa jambo hili linafanyiwa kazi,"amesema Kunenge.
Amesema kuwa,anajua wengine wamelipwa na wengine hawajalipwa kwa sababu Serikali ina utaratibu wake kwa hiyo kulipwa au kutokulipwa ni mpaka taratibu zikamilike lakini kikubwa ni kuwa na subira.
Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Zainabu Abdallah amesema, amefurahishwa na na ziara ya Mkuu wa Mkoa katika eneo hilo kwakuwa imani yake ni kupatikana kwa Suluhu ili mradi huo uendelee.
Zainabu amesema, baadhi ya wananchi waliopitiwa na mradi huo wamelipwa isipokuwa wananchi 109 bado hawajalipwa na kupelekea mkandarasi kusimama kazi ambapo amemuomba Mkuu wa Mkoa kulisimamia jambo hilo ili kusudi mradi huo upate kuendelea.
Baadhi ya wakazi wa eneo hilo akiwemo Mohamed Mataya na Juma Chanzi,wamemshukuru Mkuu huyo wa Mkoa kwa kufanya ziara kijijini hapo kwa kuwa wanaimani changamoto yao itapata majibu haraka huku wakiomba majibu yao wayapate mapema ili kusudi wajue namna ya kujipanga.