NA MWANDISHI DIRAMAKINI
KAMPENI ya Nipe Elimu Usinipe Mume inayoendeshwa na Shirika lisilo la Kiserikali la Room To Read la kumtetea mtoto wa kike imemuibua mkuu wa Mkoa wa Pwani,Abubakari Kunenge na kutaka isambazwe kwenye shule za mkoa huo.
Kunenge ameyasema hayo alipokuwa akiongea na wadau mbalimbali wakati wa uzinduzi wa Siku ya Wanawake Duniani ambapo kiwilaya ilifanyika Maili Moja Kibaha.
Amesema, kampeni hiyo ambayo inafanyika kwa wanafunzi wa kike kupitia miradi miwili ambayo ni mradi wa elimu kwa msichana na usawa wa kijinsia na usomaji na maktaba.
"Kampeni hii kupitia mradi hii ni mzuri sana na ni vizuri ukasambazwa kwa shule zote za mkoa wa Pwani ili kuhakikisha wanafunzi wa kike wanamalizia masomo yao," amesema Kunenge.
Aidha, amesema kuwa kutokana na maelezo waliyoyatoa wanafunzi wa kike ambao wako kwenye mradi huo ambapo maelezo yao yanajibu hoja ya nini kifanyike kukabiliana na vitendo vya unyanyasaji na ukatili ndani ya jamii.
"Mipango hii ni mizuri kwani itasaidia kupunguza vitendo hivyo ambapo wanafunzi wa kike wanapata stadi za namna ya kupambana na vishawishi na changamoto ili waweze kumaliza masomo na kufikia malengo yao," amesema Kunenge.
Akitoa maelezo juu ya miradi hiyo, Sifa Mkombozi alisema kuwa unahamasisha usawa wa kijinsia katika elimu ili kuhakikisha kuwa watoto wa kike wanaendelea na masomo bila kuacha kwa kusaidiana na wazazi kutatua changamoto zinazoweza kuwasababisha kuacha masomo.
Mkombozi alisema kuwa, mradi unahakikisha wanahitimu elimu ya shule ya msingi na sekondari na wanapata stadi za muhimu za kuwawezesha kufanya maamuzi ya msingi katika maisha yao.
Alisema kuwa, wanapata vitu mbalimbali kama vile madaftari, nguo na ada za shule na kupitia mradi huo Shirika linashirikisha shule, wazazi pamoja na familia katika mikutano na warsha mbalimbali zinazofanyika mashuleni.