Rhobi Samwelly:Tuendelee kuunga mkono juhudi za Serikali, wadau mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia

NA FRESHA KINASA

MKURUGENZI wa Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania linalojishughulisha na mapambano ya ukatili wa kijinsia lenye makao makuu yake Mugumu wilayani Serengeti Mkoa wa Mara, Rhobi Samwelly amesema jamii ina wajibu wa kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali na wadau mbalimbali wanaopambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia pamoja na kupigania usawa katika jamii na taifa kwa ujumla.

Rhobi ameyasema hayo leo Machi 6, 2022 wakati akizungumza na DIRAMAKINI BLOG kwa njia ya mtandao akiwa nchini Ufaransa.

Amesema kuwa, Serikali imeendelea kufanya vyema katika kuhakikisha vitendo vya ukatili vinamalizika kwa kushirikiana na wadau mbalimbali zikiwemo asasi za kiraia hivyo, ametilia mkazo wananchi kuunga mkono juhudi hizo kwa ustawi thabiti wa maendeleo kuanzia ngazi ya familia, jamii hadi taifa.
Amesema, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imeendelea kutilia mkazo ushiriki wa watu wote katika kutokomeza vitendo vya ukatili, na ndio maana imezidi kuweka msukumo chanya wa kushirikiana kwa karibu na wadau, wananchi katika maeneo mbalimbali nchini.

"Sote tumeendelea kuona namna ambavyo juhudi za Serikali na mashirika mbalimbali yanavyofanya juhudi kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia, nimpongeze Rais Samia kwa kazi nzuri ambazo ameendelea kufanya ikiwemo kuhimiza ushiriki wa wananchi katika kumaliza ukatili, na pia Waziri Mheshimiwa Dkt. Dorothy Gwajima ameendelea kuwajibika kwa nguvu zote, tumeona ziara mbalimbali akifanya katika vituo vya kulelea watoto yatima, kukutana na wadau, kukemea mila kandamizi na potofu, kuweka mikakati shirikishi ya kumaliza vitendo hivyo juhudi hizo lazima kila mmoja wetu tuziunge mkono,"amesema Rhobi.
Akizungumzia kuhusiana na maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani Machi 8, 2022, Rhobi amesema, jamii ina wajibu wa kuthamini na kutambua mchango mkubwa wa maendeleo unaofanywa na viongozi wanawake hapa nchini akiwemo Rais Samia Suluhu Hassan ambaye ni kiongozi shupavu, na muwajibikaji katika kuhakikisha taifa linazidi kupiga hatua za kimaendeleo kutokana na juhudi zake za kuleta maendeleo ambazo amekuwa akizifanya kila kukicha.

"Tanzania tuna neema kubwa kutoka kwa Mungu, Rais wetu amezidi kuliweka taifa letu katika medani nzuri za kutambulika Kimataifa, tumeshuhudia diplomasia ikistawi na ziara zake ambazo amezifanya nje zimeleta matunda kiuchumi na kijamii kwa Watanzania, amewezesha wanawake wengi kuwa viongozi ambao tunawaona wakifanya vizuri sana katika nafasi zao kuongoza kwa weledi mawaziri, wakuu wa mikoa, wilaya, wakurugenzi na maeneo mengine. hii yote ni katika kukuza usawa kwa maendeleo endelevu ya nchi yetu,"amesema Rhobi. Rhobi ameongeza kuwa, shirika analoliongoza la Hope for Girls and Women in Tanzania (HGWT) litaendelea kufanya kazi katika kuhakikisha linachagiza maendeleo ikiwemo kuweka msukumo chanya wa kuwezesha wasichana kusoma ili wafikie ndoto zao, kushirikiana na serikali kupambana na ukatili wa kijinsia pamoja na mila kandamizi ikiwemo ukeketaji, ndoa za utotoni, na aina nyingine za ukatili ambazo ni kikwazo kwa maendeleo yao.

Machi 8, 2022 ni Siku ya Wanawake Duniani, Rhobi atakabidhiwa tuzo na Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron kutokana na juhudi zake na kuthaminiwa katika mapambano ya vitendo vya ukatili wa kijinsia na kutetea haki.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news