NA FRESHA KINASA
MENEJA wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Serengeti Mkoa wa Mara, Mhandisi Deus Mchele amesema, vijiji 20 vilivyopo katika wilaya hiyo vitanufaika na huduma ya maji safi na salama kufuatia fedha shilingi bilioni 6. 2 kutolewa na Serikali kwa mwaka wa fedha 2021/2022 ili kutekeleza miradi hiyo, itakayohusisha ujenzi wa vituo 500 vya kutolea huduma ya maji.
Ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari waliofanya ziara ya kutembelea miradi mbalimbali ya maji inayotekelezwa na RUWASA katika kuhakikisha wananchi wanapata maji safi na salama.Huku fedha zilizotolewa hadi sasa akisema ni shlingi Bilioni 3.2 kati ya Bilioni 6.2.
"Upatikanaji wa maji kwa Wilaya ya Serengeti ni asilimia 59 na vijiji 26 vinapata maji kati ya vijiji 78 vya Wilaya ya Serengeti kwa fedha hizi shilingi Bilioni 6.2 tulizopata ipo miradi mingine itapanuliwa na kujengwa miradi mipya mitano katika vijiji vitano vya kata ya Nyambureti kikiwemo Kijiji cha Nyambureti, Maburi, Busuhi na Kurukerege tutafikia asilimia 67 ya upatikanaji wa maji safi na salama na jumla ya vijiji 31 ifikapo mwezi Juni,2022 baada ya miradi inayoendelea hivi sasa kukamilika," amesema Mhandisi Mchele.
Ameongeza kuwa, kwa sasa miradi hiyo inaendelea kujengwa na kwamba, kwa kipindi cha miaka miwili ijayo ni kuhakikisha wanakaribia kufikia lengo la Serikali kuwezesha upatikanaji wa maji kwa urahisi na karibu na maeneo yao kwa kumtua mama ndoo kichwani kama ilivyo dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita.
Aidha, ametaja changamoto zilizopo katika utekelezaji wa miradi hiyo kuwa ni pamoja na baadhi ya wananchi kukata mabomba, uelewa mdogo katika usimamizi wa miradi na kwamba, wanaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusiana na utunzaji wa miradi hiyo iweze kuwanufaisha kwa kipindi kirefu.
Akizungumzia mradi wa maji wa Kebanchebanche ambao ulikwama kwa muda mrefu kutokana na kutokuwa na chanzo cha maji cha uhakika, Mhandisi Mchele amesema kuwa kwa sasa mradi huo upo katika hatua nzuri baada ya kupata chanzo cha maji cha uhakika ambacho kitatoa lita za maji 8,000-10,000 kwa saa na mradi huo utawanufaisha takribani wananchi 5,000 gharama za mradi zikiwa ni shilingi milioni 700.
"Mradi upo katika hatua nzuri tayari chanzo cha maji cha uhakika kimepatikana tumechimba kisima kirefu kwenda ardhini mita 150 tayari tenki kubwa la ujazo wa lita 50,000 limekwishajengwa na mradi utakuwa na vituo sita vya kutolea huduma ya maji. Niwahakikishie wananchi kuwa, ifikapo mwezi Juni, mwaka huu mradi utaanza kuwanufaisha wananchi,"amesema Mhandisi Mchele.
Diwani wa Kata ya Kimbanchebanche, Philimoni Matiko Chacha amesema kuwa, mradi huo ukikamilika utaleta tija kwa wananchi ambao kwa muda mrefu sasa wanakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama, wakati mwingine wanatumia maji machafu katika madimbwi jambo ambalo ni hatari kwa afya zao.
"Wananchi wangu wanakwenda kuondokana na tabu kubwa ya upatikanaji wa maji safi na salama, walikuwa wakipata maji kutoka katika visima vitano vya asili ambavyo vilitobolewa na AMREF huko nyuma, lakini kutokana na uhitaji mkubwa visima hivyo vilishindwa kumudu wananchi wote na pia baadhi vilikauka, kwa hiyo maji kwa wananchi wamekuwa wakipata kwa shida, lakini kuanzishwa kwa RUWASA kumeleta mapinduzi chanya, tunaendelea kuona miradi mbalimbali wakiitekeleza kwa ufanisi mkubwa pongezi ziende kwa Rais Samia Hassan na Waziri Aweso ambao wana dhamira ya thabiti ya kumtua mama ndoo kichwani kwa kutoa fedha za miradi ya maji,"amesema Diwani Mwita.
Mradi mwingine uliotembelewa ni mradi wa maji wa Makundusi katika Kata ya Natta ambao umefikia asimia 98 na kwamba utazinduliwa hivi karibuni ukiwa umegharimu shilingi milioni 400 uanze kuwanufaisha wananchi.
Rhoda Paul Makazi wa Makundusi, akizungumzia mradi huo, amesema utakuwa mwarobaini kwa wanawake ambao walikuwa wakitembea umbali mrefu kutafuta maji na wakati mwingine kuhatarisha usalama wao kutokana na hatari ya kukutana na wanyama wakali wakati wakitafuta maji.
"Maji ni uhai na ndio nguzo ya maendeleo, nimpongeze Rais Samia kwa juhudi kubwa ambazo ameendelea kuzifanya kutenga fedha nyingi zinazogharamia miradi ya kijamii ikiwemo miradi ya maji. Mimi ninaamini kabisa mradi huu utatupa heshima kinamama, kwani tutapata maji wakati wote na kwa uhakika na ndoa zetu hazitakuwa katika migogoro kama hapo awali. Ilikuwa ukienda kutafuta maji unarudi baada ya masaa mawili hisia tofauti kwenye ndoa zinaibuka na kupelekea migogoro. wanaobedha juhudi za Rais waone haya yote anayofanya ni muhimu sana kwetu kina mama na familia zetu, tuendelee kumpa ushirikiano thabiti na kumuombea kwa Mungu,"amesema Neema Stanley.
Awali Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Mheshimiwa Dkt.Vincent Mashinji akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake amepongeza kuanzishwa kwa RUWASA kwani kumeendelea kuleta matokeo chanya hususani kuwezesha upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi wa wilaya hiyo kupitia visima virefu vinavyochimbwa na miradi mingine inayotekelezwa.
"Zipo baadhi ya changamoto ikiwemo wafugaji kukata mabomba ili mifigo yao inywe maji, naomba Wananchi wawe Walinzi na wasimamizi ya miradi hii ambayo inatekelezwa kwa faida yao. Serikali inatumia fedha nyingi lazima sasa kila mwananchi awe mlinzi wa mradi katika eneo lake. Nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kuendelea kutoa fedha ambazo kimsingi zinanufaisha na kugusa moja kwa moja maisha ya wananchi anafanya kazi nzuri sana,"amesema Dkt.Mashinji.
Pia, Dkt.Mashinji amesema RUWASA iendelee kuimarisha miradi yake upande wa miundombinu iwe imara zaidi.
Huku ndoto iliyopo akibainisha ni kuvuta maji ya Ziwa Victoria kupitia Mradi wa Mgango- Kiabakari- Butiama ambapo amesema anaamini kwamba umbali uliopo kutoka Butima kuja Serengeti si mkubwa sana ili kuwezesha upatikanaji wa maji kwa uhakika kwani wilaya hiyo in afursa kubwa ya utalii.