RUWASA yaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya maji wilayani Bunda

NA FRESHA KINASA

KATIKA kuhakikisha huduma ya maji safi na salama inaendelea kuimarika vijijini, Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA)Wilaya ya Bunda Mkoa wa Mara kwa mwaka wa fedha 2021/2022 inaendelea na utekelezaji wa miradi 15 yenye thamani ya Shilingi Bilioni 5.6.

Fedha hizo ni kutoka vyanzo mbalimbali ikiwemo fedha za UVIKO-19, P4R, PBR, na kutoka Mfuko wa Maji wa Taifa ambazo zinatekeleza miradi hiyo katika kuhakikisha ifikapo mwaka 2025 upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama vijiji unafikia asilimia 85 na mjini 95.
Meneja wa RUWASA Wilaya ya Bunda, Mhandisi William Boniface ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari wilayani humo waliofanya ziara ya kutembelea miradi ya maji inayotekelezwa.

Amesema, Wilaya ya Bunda, yenye wananchi wapatao 378,000 kati yao, wananchi 263,000 sawa na asilimia 69 ndio wanapata huduma ya maji safi na salama, lakini kutokana na miradi inayotekelezwa hivi sasa ifikapo Juni 30, 2022 watafikia asilimia 76. Huku vituo vilivyopo vinavyotoa huduma ya maji akisema ni 816.

"Kwa fedha za UVIKO-19 Bunda tumepewa Shingi Bilioni 1.5 kwa majimbo yote matatu ambapo kila jimbo limepata milioni 500, hii ni hatua muhimu sana katika kuwawezesha wananchi kupata huduma ya maji safi na salama. Rais anaendelea kufanya kazi nzuri sana kwa ajili ya Watanzania," amesema Mhandisi William.
Akizungumzia mradi wa maji wa Kibara, Mhandisi William amesema mradi huo unahudumia wananchi wapatao 21,000 na umegharimu Shilingi Milioni 558 na umekamilika mwaka 2019 ukiwa na vituo vya kutolea huduma ya maji 29. Huku Wananchi waliovuta majumbani wakiwa 247 na mapato yatokanayo na mradi huo kwa kuuza maji ndoo ya ujazo wa lita 20 kwa Shilingi 50 ni milioni 2.5 kwa mwezi.

Kwa upande wa mradi wa maji wa Karukekere umegharimu milioni 724, na unahudumia wananchi wapatao 9,000, ukiwa na vituo vya kutolea huduma 24, na wateja waliovuta maji majumbani mwao wakiwa 85 pamoja na kituo kimoja cha kunyweshea mifugo. Huku fedha ambazo zimekusanywa zilizoko katika akaunti ya mradi huo kutokana na mauzo ya maji zikiwa ni zaidi ya milioni 12.

Amesema, changamoto iliyopo katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ni baadhi ya wananchi kutokuwa na mwamko thabiti wa utunzaji wa miradi hiyo ya maji, lakini bado RUWASA wanaendelea kutoa elimu kwa jamii kutunza miradi hiyo iweze kuwanufaisha kwa kipindi kirefu.
Justina Aloyce ni mkazi wa Karukekere Wilaya ya Bunda Mkoa wa Mara ambapo amesema, uanzishwaji wa RUWASA umeleta mageuzi makubwa katika kuwaondolea wananchi changamoto ya kutembea umbali mrefu kutafuta maji.

Neema Amony amesema, hatua ya Serikali kuanzisha RUWASA kunaimarisha uhakika wa maji katika shughuli za maendeleo kwani muda mwingi ambao ungeweza kutumika kutafuta maji, unatumika kufanya shughuli za uzalishaji mali ikiwemo kilimo.

Edith Justine amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa moyo wa upendo na huruma kwa kuzidi kuimarisha huduma za kijamii kwa Watanzania ikiwemo miradi ya maji jambo ambalo amesema linapaswa kupongezwa kutokana na umuhimu wake.
Elizabeth Pius ambaye ni mkazi wa Kibara ameiomba Serikali kuendelea kupanua wigo kwa kuiwezesha RUWASA izidi kuvifikia vijiji vingi zaidi na kujenga miradi ya maji ambayo itawanufaisha wananchi.

"Faida ya kuwa na kiongozi Mkuu wa nchi ambaye ni mwanamke hakika tunaiona, ana huruma na sisi kinamama kwa sababu na yeye pia ni mama, ana upendo ndio maana tunaona akizidi kutafuta fedha nyingi kwa lengo la kutekeleza miradi mikubwa na miradi ya kijamii ambayo ina tija moja kwa moja kwa wananchi,tuzidi kumuombea kwa Mungu na kumpa ushirikiano wa kutosha azidi kuiletea maendeleo nchi yetu," amesema Yunis Jackson.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news