RUWASA yaongeza kasi kufanikisha miradi ya maji Butiama

NA FRESHA KINASA

UPATIKANAJI wa maji safi na salama katika Wilaya ya Butiama mkoani Mara ni asilimia 63 ambapo juhudi za utekelezaji wa miradi mingine saba iliyotengewa fedha Shilingi Bilioni 2.2 kwa mwaka wa fedha 2021/2022 zinaendelea na ipo katika hatua mbalimbali ili ifikapo Juni, 2022 kufikia asilimia 70 baada ya miradi hiyo kukamilika.
Hayo yamebainishwa leo Machi 11, 2022 na Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Butima, Mhandisi Dominick Mafuru wakati akizungumza na waandishi wa habari walipofanya ziara ya kutembelea miradi ya maji wilayani humo.
Mhandisi Mafuru amesema kuwa, Wilaya ya Butiama ina idadi ya wananchi wapatao 297,097 ambapo kati yao, wananchi 174,000 wanapata huduma ya maji safi na salama.
 
"Tunaendelea na utekelezaji wa miradi saba ambayo tunaamini ifikapo mwezi Juni, 2022 itakamilika kusudi tuongeze asilimia ya wananchi wanaopata huduma ya maji safi na salama ifikie asilimia 70. Kama ambavyo Serikali imedhamiria kumtua mama ndoo kichwani,"amesema Mhandisi Mafuru.
"Miongoni mwa miradi hiyo saba upo mradi wa maji Nyasurura ambao umetumia fedha shilingi milioni 150 ambao ulikuwa ni mradi wa ukarabati, mradi huu utahudumia wananchi 4,230 na una vituo 20 na maunganisho 26, sambamba na tenki lenye ukumbwa wa lita za ujazo 100,000. Hizi ni juhudi za serikali kuwaondolea usumbufu wananchi wa kupata huduma ya maji,"amesema.

Mbali na mradi huo, mradi mwingine ni mradi wa maji wa Byatika uliopo Kata ya Buhemba Wilaya ya Butiama ambao unatekelezwa kwa fedha Shilingi Milioni 663 ambao una mtandao wa kilomita 19, vituo 25 vya kutolea huduma na tenki la ujazo wa lita 135,000 unatajwa kwamba, utawawezesha wananchi kupata huduma ya maji safi na salama ambapo vijiji viwili Byatika na Kinyariri vilivyopo katika Kata ya Buhemba vitanufaika kwa sasa ulazaji wa mabomba na uchimbaji mitaro unafanyika.

Mkuu wa Wiilaya ya Butiama, Moses Kaegele akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, amesema kuanzishwa kwa RUWASA kumeleta matumaini kwa wananchi wa wilaya hiyo, kwani miradi inayoendelea kutekelezwa hivi sasa itawaondolea hadha ya kutembea umbali mrefu na kutumia muda mwingi kutafuta maji.
"Miezi saba iliyopita kulikuwepo na changamoto ya maji hapa Butiama, kulikuwa na pampu zilikuwa zimeharibika, lakini naipongeza Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan zilitolewa shilingi milioni 200 ambazo zilinunua pampu na ikafungwa, kwa sasa changamoto ya maji hapa Butiama imekwisha, hii ni hatua njema sana," amesema.

Ameongeza kuwa, kufuatia mradi Mkubwa wa Maji wa Mgango-Kiabakari- Butiama unaotekelezwa kwa thamani ya Shilingi Bilioni 70.5 amesema ukikamilka utatatua kabisa kero ya maji kwa wananchi.

Pia, amewataka wananchi kutunza miradi yote ya maji inayotekelezwa na RUWASA katika maeneo mbalimbali wilayani humo, kwani serikali inatumia fedha nyingi kwa ajili yao hivyo waitunze na kuilinda kwa manufaa endelevu.

Neema Omary Mkazi wa Byatika Kata ya Buhemba Wilaya ya Butiama amesema kuwa, kwa sasa wananchi wanatumia maji yasiyo safi na salama, lakini anaamini kwamba mradi unaotekelezwa na RUWASA ukikamilika utawakomboa wananchi kuondokana na usumbufu wa kutumia maji yasiyo safi na salama.
Zainabu Aloyce amesema, Serikali inafanya kazi kubwa ya kutekeleza miradi ya maji kwa lengo la kuwakwamua wananchi hasa maeneo ya vijijini, hatua ambayo amesema ina manufaa makubwa kwa ustawi bora wa maendeleo ya wananchi.

"Bado upatikanaji wa maji safi na salama haujawa mzuri, lakini kupitia mradi huu unaojengwa na RUWASA hapa Byatika ninaamini kabisa kwamba utatusaidia hasa sisi wanawake ambao muda mwingi hutumia kutafuta maji. Pongezi nyingi kwa Rais Samia ambaye ameona ijikite kuimarisha huduma za kijamii kwani zina manufaa makubwa zinagusa maisha yetu moja kwa moja,"amesema Aveline Pius.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news