NA FRESHA KINASA
MENEJA wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Tarime Mkoa wa Mara, Mhandisi Malando Masheku amesema kuwa, jumla ya miradi tisa ya maji yenye thamani ya shilingi Bilioni 4.33 inatekelezwa wilayani humo kwa mwaka wa fedha 2021/2022.
Lengo likiwa ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama kama ilivyo dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ilivyodhamira kumtua mama ndoo kichwani.
Amesema,miongoni mwa fedha zinazotekeleza miradi hiyo ni fedha za UVIKO-19 ambazo ni shilingi Milioni 998, fedha za Mfuko wa Maji wa Taifa milioni 534, Programu ya P4R Shilingi Bilioni 1.2 pamoja na fedha za CSR shilingi milioni 998.
"Serikali ya Rais Samia Hassan imekusudia kumtua mama ndoo kichwani, hivyo imejizatiti kutoa fedha kuyagusa maisha ya wananchi, tunayo miradi ambayo ni mradi wa maji wa Sabasaba unaotekelezwa kwa shilingi milioni 500, mradi wa maji wa Matongo shilingi milioni 998, mradi wa Mtana shilingi milioni 349, mradi wa Kitawasi shilingi milioni 389.
"Mradi wa Surubu shilingi milioni 266, mradi wa Gimenya shilingi milioni 184, mradi wa Itiryo shilingi milioni 498, mradi wa Nyangoto shilingi milioni 998 na mradi wa Sirari shilingi milioni 534 na mpaka sasa tumepokea shilingi bilioni 1.177 ukiondoa fedha za CSR na UVIKO-19,"amesema Mhandisi Malando.
Akizungumzia hali ya upatikanaji wa maji katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime Vijijini, Mhandisi Malando amesema kuwa ni asilimia 70 ambapo kwa siku mahitaji ni lita milioni 11.9 lakini kwa sasa maji yanayozalishwa ni lita milioni 8.33 na katika Halmashauri ya Tarime Mji ni asilimia 45 na juhudi mbalimbali zinaendelea kufanywa na Serikali kuongeza usambazaji wa maji maeneo ya mjini, kwani kiwango cha upatikanaji bado hakikidhi mahitaji ya wananchi.
Amesema,linachukua lita 135,000 kwani maji yanavuja yanapojaa na kwenda upande wa Kenya, hivyo akatoa ombi kwa Waziri wa Maji, Mheshimiwa Jumaa Aweso kusaidia fedha za kujenga tenki la kuhifadhia maji ujazo wa lita 300,000 huku pia akiomba changamoto ya gari la usafiri ipatiwe usumbuzi mapema kuwezesha kazi za RUWASA kutekelezeka kwa ufanisi.Kwa upande wake Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Tarime, Valentine Mganga amesema kuwa, RUWASA imeendelea kufanya kazi nzuri wilayani humo ambapo kabla ya kuanzishwa kwake miradi iliyokuwa chini ya halmashauri haikuwa na ufanisi mkubwa.
Amesema,ufanisi huo haukuwa kama ambavyo sasa RUWASA inatekeleza majukumu yake akasisitiza RUWASA kuwapa elimu wananchi wasihujumu miradi hiyo, bali wazidi kuitunza iendelee kuwanufaisha.
"Katika Wilaya ya Tarime niombe kwamba RUWASA ijitahidi kuimarisha huduma ya maji walau kufikia asilimia 75hadi 80 ifikapo 2025 ya watu watumiao maji safi na salama kwa karibu isizidi umbali wa mita 200.
"Na pia niiombe Serikali kupitia Waziri wa Maji upo mradi mkubwa wa maji wa Ziwa Victoria kupitia Rorya unakuja Tarime hadi Mgodini ambao ukitekelezwa utakuwa mwarobaini wa kumaliza shida ya maji, kuchelewa kwake kuanza ndiko kuchelewa kufikia azima ya Serikali, ziwa lile ndilo chanzo cha uhakika ili tufikie malengo chanya,"amesema Valentine.
Amesema, mradi huo utamaliza changamoto ya maji ambayo kwa sasa bado inawakabili wananchi na pia akashukuru juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan zinazoendelea kufanyika kuwezesha uimarishaji wa huduma mbalimbali za kijamii ikiwemo miradi ya maji.
Pia amesema kuwa,hatua iliyofanywa na Waziri wa Maji kuwaondoa waliokuwa wasimamizi wa RUWASA katika Wilaya ya Tarime na Mkoa wa Mara imeanza kuleta ufanisi kwani viongozi walioletwa kwa sasa wanaendelea kufanya mageuzi makubwa.
Amos Sagara ni Diwani wa Kata ya Sirari Wilaya ya Tarime ambapo ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kujenga mradi wa maji ambao unawanufaisha wananchi takribani 60,000 wa Kata ya Sirari na pia unanufaisha vijiji vingine vya Kata ya Bitiryo na Regicheri, kwani kwa siku unazalisha lita 16, 000 ambapo jumla ya watu 32,400 wananufaika na mradi huo katika vijiji sita vya kata tatu.
Sarah Yakobo ni mkazi wa Mtaa wa Mlimani Kata ya Sirari ambapo ameieleza DIRAMAKINI BLOG kuwa,mradi huo wa maji umewasaidia kuondokana na hadha ya kutafuta maji umbali mrefu na kushindwa kufanya kazi nyingine za maendeleo, lakini kwa sasa wananufaika na mradi huo.
"Nakosa jambo la kumwambia Rais wangu Samia (Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan) na Waziri wa Maji, Jumaa Aweso kwani kwa juhudi walizofanya tukapata mradi huu hakika wametukomboa kwa sehemu kubwa, kwa sasa tunapata maji muda wote na familia zetu zimeimarika, zamani ukienda kutafuta maji unatumia masaa mawili (saa mbili) au matatu (saa tatu) tena unapata maji machafu, leo hii maji ni safi na salama tunapata hapa hapa,"amesema Yasinta Denis.
Aveline Julius ameieleza DIRAMAKINI BLOG kuwa,kwa sasa binti yake anahudhuria masomo kikamilifu, ambapo awali alikuwa akihudhuria kwa kusuasua kutokana na kutumia muda mwingi kutafuta maji alfajiri na hivyo kurudi nyumbani akiwa amechelewa na kushindwa kwenda shule akihofia kuadhibiwa na walimu.
Katika Wilaya ya Tarime, miradi kadhaa inayotekelezwa wilayani humo imetembelewa na wanahabari ambapo pia wameweza kuzungumza na wananchi wanaonufaika nayo ambapo wananchi wengi wameishukuru Serikali kwa kuanzisha RUWASA ambapo wamesema inafanya kazi kubwa katika kuwapa uhakika wa huduma ya maji safi na salama.