NA FRESHA KINASA
WANANCHI wa Kijiji cha Ng'ope Kata ya Roche Wilaya ya Rorya Mkoa wa Mara wameondokana na hadha ya kutembea umbali wa kilomita 6 kwenda eneo la Olasi lililopo upande wa nchi ya Kenya kufuata huduma ya maji.
Ni baada ya Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini ( RUWASA) Wilaya ya Rorya kufanikisha ujenzi wa mradi wa maji wenye thamani ya Shilingi Milioni 120 ambao umeanza kuwanufaisha kuanzia Februari 8, 2022.
Wameyasema hayo wakati wakizungumza na waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari waliofanya ziara wilayani humo Machi 7, 2022 kutembelea miradi ya maji inayotekelezwa na RUWASA ambapo wameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwajengea mradi huo ambao wamesema, umekuwa neema kwao kwani wanapata huduma ya maji kwa uhakika wakati wote.
Magreth Odella ni mjuzaji wa maji wa Mradi wa Ng'ope ambapo amesema, kabla ya mradi huo kujengwa wanawake walitumia muda mwingi kufuata maji Olasi upande wa nchi ya Kenya umbali wa kilomita 6 kutoka katika kijiji chao na wakati mwingine ndoa zao zilikuwa katika misukosuko kwani waliamka usiku, kwa sasa wanapata maji kutoka katika mradi huo.
"Mungu amzidishie afya njema na maisha marefu Rais wetu kwa kututua ndoo kichwani kinamama, wakati mwingine tulikumbwa na vitisho njiani wakati tukifuata maji Olasi eneo la nchi ya Kenya na tulikuwa tukipata tabu sana. Fikiria ndoo moja unatumia kilomita 6, kutembea kuifuata ndipo uje ufanye kazi nyingine za uzalishaji mali, baada ya mradi huu kuanza wanawake tunanufaika na upatikanaji wa maji safi na salama kijijini hapa,"amesema Odella.
Zakayo Tito ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maji kijijini hapo amesema kuwa, kutokana na mradi huo kuanza kuwanufaisha wanawake wanashiriki katika shughuli mbalimbali za maendeleo kwani awali walitumia muda mwingi kutafuta maji wakiwemo wanafunzi na hivyo baadhi ya kushindwa kuhudhuria masomo.
"RUWASA lazima tuwapongeze wamefanya jambo zuri sana kwetu wananchi, lakini pia lazima tumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha ili wananchi tujengewe mradi huu. Hakika ni kiongozi wa mfano na wa kuigwa na namna bora ambavyo anajituma kutuletea maendeleo wananchi kwa kuyagusa maisha yetu moja kwa moja. Mradi huu tunausimamia sisi wenyewe kwa kuuza maji Shilingi 50 kwa ndoo ya lita 20 na wananchi wameupokea kwa mikono miwili na tutaendelea kuutunza uwe na tija kwa muda mrefu,"amesema Tito.
Ashura Mathias ambaye ni mkazi wa Kijiji hicho, amesema maji ni muhimu kwa matumizi ya kila siku Kwa maendelo yao na kwamba uwepo wa mradi huo umeongeza chachu kwa kinamama kuwaweka pamoja tofauti na awali ambapo kila mmoja alikuwa kivyake kutafuta maji.
James Kishinhi ni Meneja wa RUWASA Wilaya ya Rorya akizungumzia mradi wa maji wa Ng'ope amesema, mradi huo ulijengwa kwa awamu mbili mwaka 2020/2021 kwa kuchimba kisima na kuweka nishati ya umeme na kujenga bomba kuu kutokana na adha kubwa iliyokuwa ikiwakabili wananchi wa kijiji hicho ili uwe mwarobaini wa kutatua changamoto ya maji.
Ambapo kwa sasa wananchi takribani 28, 000 wanawanufaika na kwamba Serikali imetoa fedha Shilingi Milioni 78 awamu ya pili ili kupanua mtandao wa maji wa mradi kutoka eneo la Bugomba Ziwa Victoria ikiwemo kuongeza vituo vitano ili vifikie sita viwatosheleze wananchi.
"Kwa sasa wanachi wa kijiji hiki wanatumia kisima hiki kimoja, tumepewa fedha Shilingi Milioni 78 ambazo zitapanua mtandao wa maji uwafikie wananchi wengi. Asilimia ya upatikanaji wa maji ni 55, lakini hadi mwaka wa fedha uishe upatikanaji utakuwa asilimia 67 katika wilaya yetu na ifikapo mwaka 2025 tutakuwa tumefikia asilimia 85 lengo ni kuhakikisha wananchi wanapata maji Safi na Salama kama ilivyodhamira ya serikali yetu," amesema James.
Mradi mwingine uliotembelewa na wanahabari unatekelezwa na RUWASA Wilaya ya Rorya ni wa Gabimori Kata ya Kyagasanga unaotumia nishati ya sola na pampu awali ulitumia sola na invetor na uliwezeshwa na Mfuko wa Maji wa Taifa ambao ulianza mwaka 2017 ambapo kwa sasa unahudumia Wananchi zaidi ya 600 ambapo wananchi walilazimika kutembea umbali wa kilomita tatu kutoka walipo kufuata maji Ziwa Victoria.
Akizungumzia mradi huo Mwenyekiti wa Kamati ya Maji, Said Kiriga amesema kuwa mradi huo una manufaa kwa wananchi katika kuwapatia huduma bora ya maji na pia kwa sasa wanakusanya shilingi 350, 000. hadi 400, 000 kwa mwezi na juhudi za kuupanua zinafanywa na RUWASA katika kuhakikisha wananchi wanaondokana na adha ya maji.
Meneja wa RUWASA Wilaya ya Rorya, James Kishinhi amesema kuwa, Serikali imetoa fedha kupitia Programu ya EP4R kwa mwaka wa 2021/2022 Shilingi Milioni 580 kuupanua mradi huo uvifikie vijiji vingine kikiwemo Kijiji cha Manira, Nyamtinga Muharango na Kyagasaga ambapo mtandao wake utatoka Kijiji cha Gabimori kwa sasa ujenzi wa tenki kubwa la lita 150,000. la kuhifadhi maji, na kulaza mabomba unafanyika. Na kwamba, mradi utakamilika ifikapo Juni, 2022 na utawanufaisha wananchi zaidi ya 45,200 na sasa umefikia asilimia 30.
Kishinhi amesema kuwa, kwa mwaka huu wa fedha jumla ya shilingi Bilioni 3.3 zimetolewa kutekeleza miradi tisa ya maji inayoendelea kujengwa wilayani humo ambayo ipo katika hatua mbalimbali ili kuwawezesha wananchi kupata maji safi na salama.
Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini ( RUWASA) umeanzishwa chini ya Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira Namba 5 ya mwaka 2019. RUWASA ilianza rasmi shughuli zake Julai 1, 2019 makao makuu yake yakiwa jijini Dodoma.
Ambapo dira ni kuwa na Jamii ya Wananchi waishio vijijini inayopata huduma za maji safi na salama ya kutosha na ya uhakika pamoja na huduma ya usafi wa mazingira.
Dhima ya RUWASA ni kutoa huduma ya maji Safi na Salama na kuhakikisha usafi wa mazingira kwa jamii iishio vijijini kwa kufanya usanifu, ujenzi kusaidia uendeshaji wa matengenezo ya miundombinu na utoaji wa huduma kwa ajili ya kuboresha maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Huku ikisisitiza watumishi wake kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia tunu ikiwemo uadilifu, Ubunifu, Huduma bora, ushirikiano na weledi.
Baadhi ya majukumu ya RUWASA ni kufanya matengenezo makubwa ya miundombinu ya maji vijijini, kuendeleza vyanzo vya maji kwa kufanya utafiti wa maji chini ya ardhi, kuchimba visima na kujenga mabwawa, kuandaa mipango kusanifu miradi ya maji kujenga na kusimamia uendeshaji wake, kuzijengea uwezo CBWSOs kwa kutoa mafunzo na utaalamu wa uendeshaji na matengenezo ya miradi ya maji vijijini.
Majukumu mengine, ni kuhamasisha jamii na kutoa elimu ya usanifu wa mazingira katika ngazi ya kaya na masuala ya uhifadhi wa utunzaji wa vyanzo vya maji, kutafuta fedha za uendeshaji na kuiwezesha RUWASA kutekeleza majukumu yake na kushirikiana na wadau mbalimbali katika masuala yanayohusu utoaji wa huduma za maji na Usafi wa Mazingira Vijijini.