Serikali, Red Cross wafikisha elimu ya utunzaji mazingira Butiama na Rorya

*Watakiwa kuzingatia matumizi sahihi ya rasilimali ikiwemo vyanzo vya maji,hifadhi ambazo zimetengwa na serikali kama misitu, mapori ya akiba kwa matumizi endelevu

NA FRESHA KINASA

WANANCHI wa Wilaya ya Butiama na Rorya Mkoa wa Mara wanaoishi vijiji vya kandokando ya Mto Mara wameaswa kutunza mazingira na vyanzo vya maji vinavyowazunguka kwa manufaa endelevu.
Kauli hiyo imetolewa leo Machi 31, 2022 na Afisa Maendeelo ya Jamii ambaye pia ni Mratibu wa Maafa kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, Abdulatif Rajab, wakati akizungumza kwa nyakati tofauti na wananchi wa Kijiji cha Rwamisanga, Kirumi na Kitasakwa vilivyopo wilayani Butiama wakati wa utoaji wa elimu ya utunzaji wa mazingira.

Zoezi hilo la utoaji wa elimu limelenga kuvifikia vijiji nane vya Wilaya ya Butiama na Rorya ambapo limeratibiwa na Chama cha msalaba Mwekundu Mkoa wa Mara (Tanzania Red Cross Society) kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara.

Rajab amesema kuwa, ili kulinda vyanzo vya maji wananchi wanaoishi kandokando ya vyanzo vya maji wana wajibu wa kutokufanya shughuli za kibinadamu ikiwemo kilimo ambazo husababisha vyanzo hivyo kukauka.

Amesema, wananchi wana wajibu wa kuzingatia sheria za mazingira kwa kuacha mita 60 kutoka vyanzo vya maji sambamba na kushiriki kikamilifu katika upandaji wa miti katika maeneo ya vyanzo hivyo ili kuvilinda kwa ufanisi.
"Mazingira yahifadhiwe ikiwemo vyanzo vyote vya maji, Wananchi mshiriki vyema kupanda miti katika vyanzo vyote. Msifanye kazi za kilimo karibu na vyanzo kwani ni kinyume cha sheria,"amesema Rajab.

Kwa upande wake Mwezeshaji kutoka Shirika la Red Cross Mkoa wa Mara, Robinson Wangaso akizungumza katika mkutano huo, amewahimiza wananchi kuwa na maandalizi ya kujikinga na maafa kwa kuzingatia hatua muhimu katika kukabiliana na maafa ikiwemo kujiandaa kabla ya kutokea ili kuyadhibiti.
"Yapo maafa ya kiasili na yanayosababishwa na shughuli za kibinadamu. Wananchi zingatieni matumizi sahihi ya rasilimali ikiwemo vyanzo vya maji, na pia hifadhi ambazo zimetengwa na serikali kama misitu, mapori ya akiba kwa matumizi endelevu kwa maendeleo ya vizazi vijavyo na Taifa letu kwa siku za usoni,"amesema Wangaso.
Jacob Nyalusi ni Mratibu wa Red Cross Mkoa wa Mara amewaasa wananchi hao kushiriki katika utunzaji wa mazingira bila kusubiria msukumo kutoka Serikali kufanya jukumu hilo.

Jacob ameongeza kuwa, iwapo kila mmoja atashiriki kikamilifu kufanya jukumu hilo, itasaidia kwa kiwango kikubwa kuepukana na majanga ambayo yanazuilika na kuwezesha maendeleo kwa jamii na taifa pia.

Nao Wananachi wamepongeza hatua ya Red Cross Mkoa wa Mara na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara kwa uamuzi wa kutoa elimu ya utunzaji wa mazingira ambapo wamesema itawasaidia kuwajibika kikamilifu katika utunzaji wa mazingira katika maeneo yao na kuwa mabalozi kwa wengine.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news