NA MWANDISHI DIRAMAKINI
SERIKALI imetuma Maafisa walioko katika Balozi za Sweden na Ujerumani kwenda katika nchi za Poland na Hungary kufanya usimamizi na uratibu wa kuwawezesha wanafunzi hao kuvuka mpaka na kuingia katika nchi hizo kiurahisi.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) ameyasema hayo jijini Dar es Salaam alipokutana kwa mazungumzo na kamati ya wazazi wa wanafunzi wanaosoma Ukraine ili kuwatia moyo na kuelezea hatua zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali kuwezesha wanafunzi hao kurejea nchini salama.
Waziri Mulamula ameileza kamati hiyo kuwa pamoja na hatua hiyo pia Serikali inafanya mazungumzo na Ubalozi wa Urusi uliopo hapa nchini ili kuweka mazingira salama ya kuwawezesha wanafunzi wa Kitanzania waliokwama Ukraine kuondoka kwa kutumia mpaka wa Urusi kutokana na kutokuwa na njia mbadala na kuwataka wazazi kuwatuliza watoto wao wanapopata fursa ya kuzungumza nao ili kuwaepusha na taharuki.
Pia, Waziri Mulamula amewaondoa hofu wazazi wa wanafunzi takribani 160wanaosoma katika mji wa Sumy ambao uko mpakani mwa Ukraine na Urusi kwa kuwaeleza kwamba, wanafunzi hao wameshauriwa kusalia katika vyuo vyao kwa sababu za kiusalama na uongozi wa chuo chao wameahidi kuwapatia mahitaji na huduma muhimu za kibinadamu ikiwa ni pamoja na chakula,malazi na matibabu.
Waziri Mulamula ameongeza kuwa kwa sasa wanafunzi wengi wameondoka Ukraine kuelekea nchi za Poland, Romania na Hungary ambapo hadi 01 Machi, 2022, Wanafunzi 38 wamefanikiwa kuingia Poland na kupatiwa visa ya siku 55 inayowaruhusu kuwepo Poland kwa siku hizo wakati wakijiandaa kurejea nchini au kwingineko.
Pia wanafunzi 71 wamefanikiwa kuingia Hungary na kati yao 11 wameondoka kurejea Tanzania huku mmoja akisalia Hungary baada ya kukutwa na maambukizi ya UVIKO-19 na wengine wameelekea kwenye mataifa mengine kwa ndugu na jamaa zao.
Kadhalika, wanafunzi wawili wamefanikiwa kuingia Romania ambapo mmoja kati yao ameondoka kurejea Tanzania, Mwanafunzi mmoja ameingia Slovakia na Mwanafunzi mmoja Denmark.
Kwa upande wake Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolph Mkenda ameieleza Kamati ya Wazazi wa watoto wanaosoma Ukraine kuwa, Serikali itaangalia namna ya kuandaa utaratibu maalum wa kuwawezesha wanafunzi hao kuendelea na masomo wawapo hapa nchini kwa kuwa ni azma ya Serikali kupeleka wanafunzi wengi wa kitanzania kwenda nje ya nchi kusoma.
Mwenyekiti wa kamati hiyo ya wazazi wanaosoma nchini Ukraine,Wakili msomi John Choma kwa niaba ya wazazi ameishukuru Serikali inayoongozwa na Rais wa Awamu ya Sita, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa namna anavyolishughulikia suala hilo na kuwataka wazazi na watanzania kwa ujumla kuwa watulivu wakati suala hilo likifanyiwa kazi.
Tags
Kimataifa