NA MWANDISHI DIRAMAKINI
AFISA Tarafa ya Mihambwe mkoani Mtwara, Emmanuel Shilatu amefanya ziara kujionea utekelezaji wa uwepo wa mashamba kwa shule za msingi na sekondari zilizopo Tarafa ya Mihambwe ambapo ameridhishwa na kupongeza shule zote zilizotekeleza agizo hilo.
Akizungumza mara baada ya ziara hiyo, Gavana Shilatu ameeleza umuhimu wa mashamba shuleni kielimu na kiafya.
"Dhana ya mashamba shuleni yana lengo kuwapa elimu ya kilimo wanafunzi, kupunguza utegemezi na mzigo kwa wazazi, kuchochea mahudhurio na kuhakikisha upatikanaji wa chakula kwa wanafunzi shuleni wakati wote. Nimejionea mashamba yenye mazao kama vile mahindi, mihogo, kunde, alizeti, ufuta, njugu, korosho na mbaazi. Hivyo nawapongeza wote waliotekeleza ulimaji wa mazao ya chakula na mazao ya biashara,"amesema Gavana Shilatu.
Wakati huo huo, Gavana Shilatu amekagua utekelezaji wa zoezi la anuani za makazi ambapo ameona vibao barabarani, nyumba zikiwa na namba na kutoa maelekezo zoezi likamilishwe vyema na kwa wakati.
Katika ziara hiyo Gavana Shilatu alitembelea Shule ya Msingi Mitondi na kutembelea maeneo mbalimbali huku akiambatana na uongozi wa Halmashauri ya Serikali ya Kijiji Mitondi B, uongozi wa shule pamoja na viongozi wa CCM kukagua utekelezaji wa ilani ya uchaguzi.