NA MWANDISHI MAALUM
AFISA Tarafa ya Mihambwe mkoani Mtwara, Emmanuel Shilatu amefanya ziara kujiridhisha uhalisia wa upatikanaji wa chakula kwa wanafunzi wote wa shule za msingi na sekondari zilizopo Tarafa ya Mihambwe ambapo ameridhishwa na upatikanaji huo wa chakula lishe kwa wanafunzi.
Gavana Shilatu alijionea uhalisia wa wanafunzi wakipewa kifungua kinywa, chakula cha mchana na chakula cha usiku kwa wa walio hosteli ambapo alitoa pongezi kwa hatua hiyo kubwa ya uzingatiaji lishe kwa wanafunzi.
"Napenda niwapongeze wazazi na walimu kwa namna wanavyoendelea na utaratibu wa kuzingatia suala la lishe kwa wanafunzi. Upatikanaji chakula unaimarisha elimu na afya kwa mtoto. Ni jukumu la kila mdau wa elimu kuhakikisha lishe inazingatiwa kwa wanafunzi kutokana na umuhimu wake," amesema Gavana Shilatu mara baada ya ziara.
Serikali ilitoa mwongozo kupitia Wizara ya Elimu kuhakikisha wanafunzi wote wanapatiwa lishe shuleni kwa ajili kuimarisha elimu na afya. Jambo ambalo linatekelezwa vyema kwa shule zote za msingi na sekondari zilizopo Tarafa ya Mihambwe.