NA MWANDISHI DIRAMAKINI
MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu, Simba SC wameilaza Dodoma Jiji FC mabao 2-0 katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara.
Ni kupitia mtanange uliopigwa katika dimba la Benjamin Mkapa lililopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, Dar es Salaam usiku wa Machi 7, 2022.
Mabao ya Simba yamefungwa na kiungo Mzambia, Clatous Chama dakika ya 56 kwa penalti na mshambuliaji Mnyarwanda, mzaliwa wa Uganda, Meddie Kagere dakika ya 74.
Dakika 45 za kwanza, Dodoma Jiji walionekana kuwa wagumu, hivyo Simba walianza mchezo kwa kasi na kupiga pasi fupifupi kuelekea lango la wapinzani wao na kutengeneza nafasi kadhaa.
Aidha,uimara wa safu ya ulinzi ya Dodoma Jiji ikiongozwa na beki kisiki George Amani Wawa iliwanyima nafasi ya kuandika bao la kuongoza.
Dodoma Jiji walionekana kuingia na mbinu za hali ya juu kucheza kwenye eneo lao la ulinzi na kufanya mashambulizi ya kushtukiza kupitia mshambuliaji Seif Karihe ambaye alishindwa kutamba mbele ya walinzi wa Simba SC.
Nahodha John Rafael Bocco alishindwa kuendelea na mchezo dakika ya 28 na nafasi yake kuchukuliwa na Meddie Kagere.
Hata hivyo, kipindi cha pili Simba SC walirejea kwa kasi na iliwachukua dakika 12 tu kuandika bao la kwanza kupitia kiungo Clotus Chama kwa mkwaju wa penati baada ya mlinzi George Wawa kuunawa mpira katika eneo la hatari na dakika 75 Meddie Kagere akaandika bao la pili.
Ndani ya dimba hilo,mashabiki wa Simba SC walionekana kuwa na furaha baada ya kuwaona wachezaji wao Thadeo Lwanga na Kibu Denis wakirejea uwanjani baada ya kukosekana kwa muda mrefu kutokana na kuwa majeruhi.
Kwa ushindi huo, timu ya kocha Mspaniola, Pablo Franco Martin inafikisha alama 37, ingawa inabaki nafasi ya pili, ikizidiwa alaam nane na watani wao Yanga SC baada ya wote kucheza mechi 17.
Awali katika mechi zilizotangulia, Ruvu Shooting imelazimishwa sare ya 0-0 na Biashara United Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani.
Nao Coastal Union imewachapa wenyeji KMC 2-3 Uwanja wa Azam Complex, Chamazi katika Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, Dar es Salaam.
Mabao ya Coastal Union yamefungwa na Abdul Hamisi kwa penalti dakika ya 22, William Kisingi dakika ya 82 na Rashid Chambo dakika ya 90.
Kwa upande wa KMC yamefungwa na Emmanuel Mvuyekure dakika ya 40 na Kenny Ally dakika ya 47 ya mtanange huo.
Tags
Michezo