NA MWANDISHI DIRAMAKINI
WAWAKILISHI pekee wa Tanzania katika michuano ya Kimataifa, Simba SC wamechapwa mabao 3-0 na wenyeji ASEC Mimosas katika mchezo wa Kundi D Kombe la Shirikisho barani Afrika.
Ni kupitia mtanage uliopigwa leo Machi 20, 2022 katika dimba la Jénérali Mathieu Kerekoumjini Cotonou nchini Benin.
Aubin Kramo Kouamé dakika ya 16, Mburkina Faso, Stephane Aziz Ki dakika ya 25 na mshambuliaji Karim Konaté dakika 57 ndiyo waliosababisha maumivu kwa Simba SC.
Aidha,Aishi Salum Manula alifanikiwa kuokoa mikwaju miwili ya penalti ya Konaté dakika ya 36 na mshambuliaji mwingine, Anicet Alain Oura dakika ya 90.
Matokeo haya yanaifanya ASEC kufikisha alama tisa na kupanda kileleni kwa Kundi D, ikizizidi alama mbili Simba na RSB Berkane ya Morocco.
Huku US Gendamarie ikiendelea kushika mkia sasa kwa kufikisha alama tano baada ya wote kucheza mechi tano kuelekea mechi za mwisho siku chache zijazo.
ASEC wanatarajiwa kumalizia ugenini dhidi ya Berkane, Simba SC watamalizia nyumbani na US Gendamarie kuwania nafasi mbili za juu ili kwenda Robo Fainali.
Hata hivyo, Simba SC imeahidi kufanya kila liwezekanalo ili kuhakikisha inasonga mbele kupitia mtangange ujao.